Wednesday, June 4, 2014

Aliyekuwa mgombea wa nafasi ya urais klabuni hapo, Michael Wambura.

MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zakaria Hans Pope, amesema kwa sasa hataki kujihusisha na masuala ya usajili, badala yake ataelekeza nguvu zake katika biashara zake binafsi.
Mwenyekiti huyo ameitoa kauli hiyo hivi karibuni wakati klabu mbalimbali zikiendelea na usajili kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na sababu kubwa ni uchaguzi lakini zaidi amemtaja aliyekuwa mgombea wa urais katika uchaguzi mkuu wa klabu hiyo, Michael Wambura.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zakaria Hans Pope.
Akizungumza na Championi Jumatano, Hans Pope alisema kwa sasa hataki kujihusisha na usajili wa timu hiyo, badala yake anawaachia viongozi wapya watakaoingia madarakani.
Hans Pope amefunguka kuwa ni ngumu kwake kumfanyia usajili kiongozi ambaye hadi sasa hamjui, kwa kuwa miongoni mwa wagombea, wapo ambao hana maelewano nao mazuri.
Ameeleza kuwa alichokifanya ni kufanya mazungumzo na baadhi ya wachezaji ambao mikataba yao imemalizika kwa ajili ya kuwaongezea mingine kwa mujibu wa ripoti ya kocha, Zdravko Logarusic.
“Itawezekana vipi nifanye usajili wa wachezaji wapya nikiwa sielewani na baadhi ya wagombea wa uchaguzi Simba na mbaya zaidi ikitokea ambaye sielewani naye akashinda!
“Mfano halisi leo hii Wambura (Boniface) ashinde urais, unafikiri kutakuwa na maelewano mazuri kati yangu na yeye? Ninajua ameondolewa kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi, lakini amekata rufaa TFF, itakuwaje kama akishinda rufaa na kuingia kwenye uchaguzi?” alihoji Hans Pope na kuongeza:
“Mbaya zaidi itokee kuwa usajili tutakaoufanya wa wachezaji kwa ajili ya msimu ujao, timu ikafanye vibaya, maneno mabaya tutaambiwa, hivyo mimi nimejitoa kwenye usajili.”
Hans Pope ni mmoja wa wadau wa klabu hiyo ambao walikuwa mstari wa mbele kufanya usajili msimu uliopita, ambapo alitumia zaidi ya shilingi milioni 100 kwa ajili ya kufanya usajili kwa wachezaji wapya na kuboresha mikataba ya wale waliokuwa wamemaliza mikataba yao ya awali.

0 comments:

Post a Comment

Designed by Adamu Mwanakatwe