Saturday, June 28, 2014

Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Mganda, Emmanuel Okwi.

IMEFAHAMIKA kuwa, kiungo mshambuliaji wa Yanga, Mganda, Emmanuel Okwi, ameuomba msamaha uongozi wa timu hiyo na kuomba mwenyewe kurejea Jangwani.
Hiyo ni baada ya kusikia taarifa za kupunguzwa kwa mkataba wake kutokea miaka miwili hadi mwaka mmoja kutokana na kushindwa kutimiza wajibu.

Yusuph Manji akiwa na wapenzi, washabiki na wanachama wa klabu ya Young Africans.
Okwi alipata taarifa hizo kupitia mwanasheria wake, Edgar Agaba katika kikao walichokaa na Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji, hivi karibuni.
Wakati mkataba wake ukipunguzwa, zipo tetesi kuwa upo uwezekano mkubwa wa kiungo huyo kutemwa katika kikosi hicho kinachojiandaa na Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho Afrika.
Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka ndani ya kamati ya utendaji ya timu hiyo, simu nyingi wanapokea kutoka kwa kiungo huyo akiomba msamaha.
Chanzo hicho kilisema, mwanasheria wake hivi sasa anapambana kuhakikisha mkataba wake unabakia kama ilivyosainiwa mwanzoni wa miaka miwili.
“Okwi hivi sasa anapiga simu mwenyewe tofauti na ilivyokuwa mwanzoni alipokuwa akipigiwa simu hapokei na wakati mwingine anaizima kabisa.
“Lakini hivi sasa anapiga simu kila wakati kwa viongozi wa Yanga akiomba msamaha na kutaka mkataba wake kubakizwa kama ilivyokuwa mwanzoni, pia arejee kuichezea Yanga baada ya kupewa taarifa za kupunguzwa kwa mkataba wake,” kilisema chanzo hicho.
Hivi karibuni Manji alitangaza kutumia kiasi chochote cha fedha kwa ajili ya kumleta mbadala wa Okwi kwa ajili ya kuichezea timu hiyo katika msimu ujao.

0 comments:

Post a Comment

Designed by Adamu Mwanakatwe