Saturday, June 28, 2014

Coutinho akiwa katika pozi.

KIUNGO mshambuliaji wa Kibrazili, Andrey Coutinho, aliyetua jana (Ijumaa), kutoka nchini humo kuja kukipiga kwenye timu ya Yanga, jana alitua na mkosi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), jijini Dar es Salaam, baada ya gari lililoenda kumchukua kufungwa nyororo na wasimamizi wa maegesho ya magari uwanjani hapo.
Katika sakata hilo mchezaji huyo baada ya kutua uwanjani, alipokelewa na viongozi na mashabiki wa timu hiyo wakiwemo Meneja wa timu hiyo, Afidh Saleh, Msemaji, Baraka Kizuguto, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya timu hiyo, Mohammed Binda na viongozi wengine na mashabiki wa timu na kuongozwa moja kwa moja kwenye gari aina ya Toyota Alteza aliloandaliwa kumpeleka kwenye klabu ya timu hiyo.
Muda mfupi kabla ya mchezaji huyo kuingia kwenye gari hilo, kundi lililokwenda kumpokea mchezaji huyo liligundua kuwa gari hilo limefungwa nyororo na wasimamizi wa maegesho ya uwanja huo hivyo kushindwa kuondoka.


Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Mohammed Binda (kushoto), akiwa akiwa na Coutinho baada ya kuwasili uwanjani hapo.
Kitendo hicho kilisababisha mchezaji huyo kupigwa na butwaa lakini akaamua kuingia ndani ya gari hilo na kujipumzisha wakati viongozi wa Yanga wakihaha kuwasaka waliolifunga gari hilo.
Akizungumza na Championi wakati sakata hilo likiendelea msemaji wa timu hiyo (Kizuguto), alisema anashangaa wasimamizi wa maegesho hayo kulifunga nyororo gari lao wakati sehemu waliyopaki waliekezwa na afisa mmoja wa polisi mwenye nyota moja.
“Mimi nawashangaa hawa jamaa, sisi tusingeweza kupaki hapa bila kuelekezwa, kuna afisa mmoja wa polisi mwenye nyota moja ndiye aliyetuelekeza tupaki hapa tena ndiye yule aliyeongoza mapokezi ya Maximo jana (Alhamisi), mbona hata gari lililomchukua Maximo nalo lilipaki hapahapa?” Aliuliza Kizuguto huku akilalamika.

Msemaji wa Yanga, Baraka Kizuguto (wa tatu kutoka kushoto) akimuongoza mchezaji huyo baada ya kumpokea uwanjani hapo. Wengine ni mashabiki wa Yanga waliofika uwanjani hapo kukipokea ‘kifaa hicho’.
Wakati Kizuguto akisema hayo kundi la mashabiki wa Yanga waliofika kwenye mapokezi, lilikuwa likipiga mayowe na kusema aliyelifunga gari hilo ni lazima atakuwa ni mtu wa timu ya Simba na alifanya hivyo makusudi maalum kwani baada ya kulifunga gari mtu huyo alipotea ambapo juhudi za kumsaka zilichukua zaidi ya dakika ishirini.
Baada ya sakata hilo kutaka kuleta sura ya vurumai kutoka kwa mashabiki waliokuja kumpokea mchezaji huyo baadhi ya maofisa wa uwanja huo walikubaliana kulifungulia gari hilo ambapo faini yake ya kuegesha sehemu hiyo ingegharimu shilingi elfu ishirini.

0 comments:

Post a Comment

Designed by Adamu Mwanakatwe