
Maximo (katikati) akiwa na kocha msadizi wa Yanga, Mbrazili Leornado Leiva Martins (kulia).
KOCHA Mkuu wa Yanga, Mbrazili, Marcio Maximo, amekabidhi mapendekezo ya usajili kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara huku akitaka wachezaji wenye uwezo wa kimataifa.
Mbrazili huyo alitua juzi Alhamisi jijini akiwa ameongozana na msaidizi wake, Leornado Leiva kwa ajili ya kukinoa kikosi hicho kinachojiandaa na Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho Afrika.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Maximo alisema kuwa katika usajili wa wachezaji wake lazima uwepo mchanganyiko wa mataifa mbalimbali, ikiwemo Ulaya.
Maximo alisema, lengo la usajili huo ni kutengeneza kikosi imara na chenye uwezo wa kucheza mashindano ya kimataifa ili wafanye vizuri.
Aliongeza kuwa, katika kukiimarisha kikosi amepanga kutengeneza msingi mzuri wa kuwandaa wachezaji kwa kuunda kikosi imara cha U20 kitakachokuwa chini ya msaidizi wake, Leiva.
Pia amepanga kuanza kukinoa kikosi hicho keshokutwa Jumatatu kwa kuanza na programu ya mazoezi ya nguvu.
“Tayari nimekabidhi mapendekezo ya usajili wangu kwa Kamati ya Utendaji ya Yanga, kikubwa ninataka wachezaji wenye uwezo wa kucheza mashindano ya kimataifa.
“Katika usajili wangu lazima uwepo na mchanganyiko wa wachezaji kutoka mataifa mbalimbali kwa kuanzia Afrika na Ulaya.
“Lengo ni kuleta mchanganyiko wa aina ya soka kutoka mataifa mbalimbali, haiwezekani timu iundwe na wachezaji Watanzania pekee, alisema Maximo na kuongeza:
“Kwa nini TP Mazembe yenyewe iwe inajulikana kimataifa? Haiwezekani, hivyo lazima na sisi tufikie historia nzuri kama waliyokuwa nayo hao kwa kuchukua makombe mbalimbali Afrika.”
Aidha, aliongeza kuwa, anaufahamu vizuri ushindani wa ligi uliopo ambapo hivi sasa umeongezeka, hasa kutoka kwa timu za Azam FC, Mbeya City, Kagera Sugar na Mtibwa Sugar.
Alipoulizwa Katibu Mkuu wa Yanga, Beno Njovu kuhusiana na mapendekezo hayo, alisema: “Ni kweli tumepokea mapendekezo ya usajili wa wachezaji anaowataka Maximo, tayari yamefika kwa uongozi mapendekezo yake hayo.
“Ripoti hiyo tumeipitia, lakini tutaangalia kama mapendekezo hayo yataambatana na kanuni za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).”
Katika hatua nyingine baada ya kutambulishwa rasmi, Kocha Mkuu wa Yanga, Mbrazili, Marcio Maximo, amefunguka kuwa hana ugomvi wowote na kipa wa timu hiyo, Juma Kaseja.
Maximo ambaye alikuwa kocha wa Taifa Stars miaka kadhaa iliyopita, aliwahi kutofautina na kipa huyo ambaye alikuwa Simba lakini hakuna kati yao ambaye aliwahi kueleza ukweli wa kilichotokea.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Maximo alisema ugomvi baina yake na kipa huyo umeisha na hakuna tatizo lolote, kinachofuata sasa ni kazi tu.
Maximo aliongeza kuwa, kama ni ugomvi na kipa huyo ulikuwepo zamani lakini hivi sasa hakuna tena kitu hicho, badala yake watashirikiana kwa pamoja katika kuijenga Yanga imara.
Aliongeza kuwa, pia angemkuta kiungo mkabaji wa timu hiyo, Athumani Idd ‘Chuji’ ambaye ameondolewa kikosini hivi karibuni, asingekuwa na ugomvi naye.
“Ninaamini na kuheshimu uwezo wa Kaseja, kwangu ni kipa bora hapa nchini, ni vyema ikafahamika hilo, pia ijulikane kuwa sina ugomvi na mchezaji yeyote akiwemo Kaseja na Chuji.
“Kama ni ugomvi wangu na Kaseja na Chuji ulikuwepo zamani, lakini siyo hivi sasa, Kaseja nilimfukuza nikiwa naifundisha Stars, hivi sasa nipo Yanga,” alisema Mazimo na kuongeza:
“Mimi na Kaseja tutaendelea kufanya kazi pamoja, mimi na yeye tunatakiwa kupita njia moja iliyo sahihi ili timu ifanikiwe katika mashindano mbalimbali.”
0 comments:
Post a Comment