Thursday, June 26, 2014


 

WAKATI beki wa Italia, Giorgio Chiellini akifura kwa hasira baada ya kung’atwa na mshambuliaji wa Uruguay, Luis Suarez juzi Jumanne katika mechi ya fainali za Kombe la Dunia, hali ni tofauti nje ya uwanja.
Ripoti zinadai kwamba wacheza kamari wa nchi za Scandinavia walilifurahia tukio hilo kwa madai kwamba walichokibashiri kimeibuka kuwa kweli.
Kampuni ya kamari kwa njia ya mtandao ya Betsafe, walitangaza kwa wacheza kamari kwamba Suarez ambaye alifungiwa kwa kung’ata wachezaji mara mbili atafanya hivyo tena kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil.
Inadaiwa kwamba zaidi ya wachezaji kamari 100 walisimamia katika hoja hiyo na ilipotokea kwa Suarez kumng’ata Chiellini begani kwao ilikuwa wakati wa kulifurahia tukio hilo.
Mshindi mmoja, Jonathan Braeck kutoka Stenungssund, Sweden, katika dau lake aliweka Dola 12.4 akisema kwamba Suarez atang’ata mchezaji mwenzake na Braeck sasa anasubiri malipo mazuri.
“Awali nilikuwa na fikra za kuweka fedha nyingi lakini rafiki yangu mmoja aliniambia kwamba ninapoteza fedha zangu,’’ alisema Braeck katika mazungumzo na Gazeti la SportExpressen.
“Italia ilipotawala mchezo katika hali ya kawaida unajua kwamba atakuwa na uchizi fulani, sikufikiria angeng’ata mtu lakini angefanya jambo la kipumbavu kilichotokea ni kwamba alifanya jambo la kipumbavu zaidi,’’ alisema.
Betsafe walithibitisha ushindi wa Braeck kupitia Meneja Masoko wao, Patrik Oqvist kwa kusema: “Tunaweza kuthibitisha kwamba mteja wetu ameshinda fedha za Sweden Korona 14,000 kwa sababu kwa mara nyingine, Suarez alimng’ata mchezaji wa timu pinzani.’’
“Tuliliweka hili katika hali ya mzaha lakini inafurahisha kwamba mmoja wa wateja wetu amekuwa sahihi,’’ alisema Oqvist.
Braeck alisema kwamba anatarajia kutumia fedha alizopata kwenda England kushuhudia mechi za Ligi Kuu lakini hatokwenda Liverpool kuonana na mtu aliyesaidia kufanikisha safari yake.
“Itakuwa ni safari ya Manchester. Najaribu kutafuta mtu ambaye nitakwenda naye Mancheter United,” alisema.
“Kama nitaipata anuani ya nyumbani kwa Suarez nitamtumia kadi ya shukurani, ilikuwa jambo zuri kwake kumng’ata mtu na kunipa safari ya Manchester.”

0 comments:

Post a Comment

Designed by Adamu Mwanakatwe