
KAMBI ya mmoja wa wagombea urais wa Simba, imeunda kamati ya
usajili ambayo imeshafanya mazungumzo na wachezaji 35, lakini watachuja
mpaka wabakie 12 na moja kati ya masharti iliyojiwekea ni kutomsajili
mchezaji yeyote kutoka Yanga.
Jopo hilo ambalo linakutana mara kwa mara na
kufanya shughuli zake kwa usiri mkubwa, linahusisha baadhi ya wajumbe
waliopo kwenye kamati ya usajili ya sasa ya Simba ambao wanaamini kwamba
mgombea huyo huenda akaingia madarakani.
Mmoja wa viongozi wa kamati hiyo ambaye hakupenda
kutajwa jina lake gazetini kwa kuhofia kuwa lolote linaweza kutokea
kwenye uchaguzi, alisema wameamua kufanya mchakato huo mapema ili
wakiingia madarakani wasipate shida.
Tayari wameshazungumza na wachezaji 35 ambao wote
wamekubali kujiunga na Simba lakini wenyewe watawachuja hadi kufikia 12
inayowahitaji kujumuisha na wale waliopo sasa kikosini.
Kamati hiyo imezungumza na kukubaliana kila kitu
na wachezaji hao lakini mambo yakigeuka kila kitu kinawekwa pembeni.
Katika vikao vyao vyote, kamati hiyo wamesisitizana kutosajili mchezaji
yeyote kutoka Yanga kwani wanaamini wengi wanakuwa mamluki na huwa
hawachezi kwa kujituma inapofikia timu inahitaji ushindi wa lazima.
“Lakini hatuwezi kuwasajili hadi uchaguzi upite,
kama kambi yetu ikishinda mambo yataendelea kama yalivyopangwa lakini
kinyume na hapo wataishia kuzungumza tu na viongozi wa Simba,
hawataichezea Simba,” alisema mmoja wa viongozi wa kamati hiyo ambaye
amewahi kusajili wachezaji wa Simba mara kadhaa.
Wachezaji wa Yanga waliomaliza mikataba yao ambao
wanatajwa kuwa na mipango ya kujiunga na Simba ni kipa Ally Mustapha
‘Barthez’na beki wa kushoto David Luhende. Wote hao ni hitaji la Kocha
Zdravko Logarusic ambaye katika ripoti yake ameusisitiza uongozi
kusajili kipa atakayempa changamoto Ivo Mapunda na beki wa kushoto wa
uhakika.
Banda naye aingia kundini
Katika mlolongo wa wachezaji hao wanaosajiliwa
yumo beki wa Coastal Union, Abdi Banda, ambaye pia awali alikuwa
akiwindwa na Yanga. Meneja wa mchezaji huyo Abdul Bosnia, alisema kuwa
mazungumzo na mgombea mmoja wa nafasi ya juu kwenye uongozi wa Simba
yanakwenda vizuri ingawa walimtaka amalizane na uongozi wa Coastal kwani
mchezaji huyo bado ana mkataba wa mwaka mmoja.
“Kuna kiongozi wa Simba (anamtaja mgombea huyo)
tunafanya naye mazungumzo kuhusu usajili, tumemwambia aonane na viongozi
wa Coastal ambao ndiyo wamiliki wa mchezaji huyo, kila kitu kipo sawa
hata ofa tuliyopewa ni nzuri ingawa tunajaribu kuiangalia zaidi.
“Banda ni mchezaji ambaye anaruhusiwa kuichezea
timu yoyote, hata Yanga walikuwa wanamtaka ingawa kocha wao alimkataa
ila mpaka leo (jana asubuhi) kuna kiongozi amenipigia kuuliza kama Simba
wamemalizana na sisi,” alisema Bosnia.
0 comments:
Post a Comment