
Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu.
SASA muziki umekalimika. Mastraika wa Tanzania wanaochezea TP Mazembe ya DR Congo Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanawasili kesho Jumamosi kujiunga na Taifa Stars kwa ajili ya mechi dhidi ya Zimbabwe itakayochezwa keshokutwa Jumapili Uwanja wa Taifa.
Washambuliaji hao watatokea moja kwa moja Sudan ambapo leo Ijumaa TP Mazembe itacheza mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Hilal.
Ujio wa washambuliaji hao utafanya wachezaji wote kutoka nje walioitwa na Kocha Mart Nooij kutimia kwa ajili ya mechi hiyo ya mchujo ya Kombe la Afrika 2015 ambalo fainali zake zitachezwa Morocco. Mchezaji mwingine wa nje ambaye tayari ameripoti Taifa Stars ni Mwinyi Kazimoto anayecheza nchini Qatar.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeishukuru TP Mazembe kwa kuwaruhusu wachezaji hao kujiunga na Taifa Stars kwa kuwa wataiongezea nguvu safu ya ushambuliaji ambayo haina makali.
Wakati huo huo, Zimbabwe inawasili leo Ijumaa usiku ikiwa na msafara wa watu 27. Timu itafanya mazoezi siku hiyo jioni kwenye Uwanja wa Taifa tayari kwa mechi hiyo itakayochezwa Jumapili saa 10 kamili jioni kwenye uwanja huo.
0 comments:
Post a Comment