
Okwi alisaini mkataba wa dola 100,000 ambazo ni zaidi ya Sh160 milioni lakini Yanga ilimpa kianzio cha dola 60,000 (Sh96 milioni) hivyo sasa anadai dola 40,000 (Sh64 milioni) na hapo ndipo sekeseke lilipo.
UNAIKUMBUKA kauli ya Mwenyekiti wa klabu hiyo, Yusuf Manji,
kumhusu nyota wao, Emmanuel Okwi? Sasa imepata majibu kutoka kwa
Mwanasheria wa mchezaji huyo, Edgar Aggaba, aliyesema: “Acheni mchezo,
sisi tunataka fedha zetu tu.”
Ishu ni fupi sana, Manji wakati anazungumza na
waandishi wa habari Jumapili iliyopita alisema mambo mengi, lakini
aligusia sakata la Okwi na klabu hiyo ambapo alisema: “Okwi tulimpa
mkataba wa miaka miwili na nusu huku tukikubaliana tufuatilie hati ya
uhamisho wake ili aichezee Yanga, ila ilichelewa na akakosa baadhi ya
mechi, lakini baadaye akajitoa katika timu bila kuutaarifu uongozi
akitaka amaliziwe fedha zake ndiyo aendelee kuichezea Yanga.
“Sasa kutokana na hali hiyo ya kushindwa kuichezea
Yanga baadhi ya mechi, inabidi achague ama kuongeza mkataba wake hadi
miaka mitatu au sehemu ya fedha anayodai ikatwe.”
Okwi alisaini mkataba wa dola 100,000 ambazo ni
zaidi ya Sh160 milioni lakini Yanga ilimpa kianzio cha dola 60,000 (Sh96
milioni) hivyo sasa anadai dola 40,000 (Sh64 milioni) na hapo ndipo
sekeseke lilipo.
Lakini akizungumza na Mwanaspoti akiwa Uganda,
Aggaba alisema ameisikia kauli ya Manji kuhusiana na mteja wake Okwi,
hata hivyo akasisitiza kwamba amekubaliana na mchezaji huyo kukaa meza
moja na Yanga kuzungumza juu ya kukosa mechi sita, lakini kwanza alipwe
fedha zilizobaki.
Aggaba alisema Yanga inatakiwa kumlipa kwanza Okwi
fedha zake ambazo ahadi ya kumlipa mapema siku chache baada ya kutua
nchini ndiyo iliyotangulia vinginevyo watakuwa na uamuzi mwingine juu ya
mkataba wa mchezaji huyo.
Mwanasheria huyo alisema atazungumza na Okwi
ambaye leo (Ijumaa) asubuhi alikuwa safarini na kikosi cha Uganda ‘The
Cranes’ kuelekea Madagascar kucheza mechi ya kuwania tiketi ya fainali
za Kombe la Mataifa ya Afrika.
Alisema endapo Yanga itashindwa kumlipa fedha zake hadi Juni 30 mwaka huu wataanza mchakato wa kuvunja mkataba.
“Hapa kuna mambo mawili, la kwanza ni Okwi kulipwa fedha zake za usajili, hilo ndiyo lililotangulia.
Pia ni Yanga kutaka wafidiwe baada ya Okwi kukosa
mechi za mwanzo, kama wanataka tuzungumze hakuna shida, lakini nafikiri
kwanza wanatakiwa kukamilisha jambo la kwanza ambalo ni malipo ya
mchezaji ambayo tulikubaliana wakati anasajiliwa kuwa akifika Tanzania
atalipwa haraka,” alisema Aggaba.
“Yanga wanatakiwa kukumbuka kwamba Okwi hakujizuia
kuichezea Yanga, ni matatizo ya huko Tanzania kutojua kanuni ndiyo
yaliyomfanya ashindwe kuichezea timu, nitazungumza na Okwi akirudi
Madagascar na kama Yanga hawatamlipa mpaka kufika mwisho wa mwezi Juni
mwaka huu tutaangalia la kufanya likiwamo la kuvunja mkataba.”
Okwi alikosa mechi tatu za kwanza za mzunguko wa
pili wa Ligi Kuu Bara msimu uliomalizika hivi karibuni dhidi ya Ashanti
United, Coastal Union na Mbeya City pia ile ya Ligi ya Mabingwa Afrika
dhidi ya Komorozine de Domoni ya Comoro kutoka na utata wa usajili wake.
0 comments:
Post a Comment