Thursday, May 15, 2014

“Mwenendo huu ni wa kipekee na upo Tanzania tu na hautumiki mahali popote katika jumuiya ambazo Tanzania ni mwanachama wake na hata nchi yoyote duniani,” alisema CAG Utouh katika ripoti hiyo na kuongeza: “Nimerudia pendekezo hili kwa miaka mitano mfululizo bila kutekelezwa na mamlaka husika.”

Dodoma. Mapendekezo ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ya kuitaka Serikali kutowateua wabunge kuwa wajumbe wa bodi za mashirika ya umma, hayajatekelezwa kwa miaka mitatu mfululizo.
Ripoti ya CAG ya ukaguzi wa mashirika ya umma kwa mwaka 2013/2014 iliyowasilishwa bungeni mjini Dodoma imesema mapendekezo hayo yaliwasilishwa kwa mara ya kwanza 2008/2009.
Katika ripoti hiyo, CAG Ludovic Utouh amesema katika mkutano wa uwajibikaji uliofanyika Januari 23 na 24, 2009 iliamuliwa kuwa wabunge ambao ndiyo wasimamizi wa sheria kikatiba, wasiteuliwe kuwa wajumbe wa bodi za mashirika ya umma.
“Mwenendo huu ni wa kipekee na upo Tanzania tu na hautumiki mahali popote katika jumuiya ambazo Tanzania ni mwanachama wake na hata nchi yoyote duniani,” alisema CAG Utouh katika ripoti hiyo na kuongeza: “Nimerudia pendekezo hili kwa miaka mitano mfululizo bila kutekelezwa na mamlaka husika.”
Kisheria, Rais huteua mwenyekiti wa bodi husika na waziri mwenye dhamana huteua wajumbe.
Aidha, CAG alisema kanuni za utawala bora zinataka watendaji wakuu wa mashirika ya umma wateuliwe na bodi za wakurugenzi wa mashirika hayo badala ya kazi hiyo kufanywa na Rais.
“Ili kumpunguzia mzigo Mheshimiwa Rais, ninashauri angeachiwa jukumu la kuteua wenyeviti wa bodi za wakurugenzi wakati uteuzi wa maofisa watendaji wakuu liwe ni jukumu la bodi,” alisema.
CAG alisema mfumo huo utaziwezesha bodi za wakurugenzi kuziwajibisha menejimenti za mashirika ya umma pale viongozi hao watakaposhindwa kuwajibika ipasavyo.

0 comments:

Post a Comment

Designed by Adamu Mwanakatwe