
Mtoto wa marehemu aliyeokolewa katika ajali hiyo akiwa na shangazi yake
Mvua inaweza kuwa neema pale inaponyesha kwa
wastani, lakini ikawa karaha pale inapokuwa kubwa, hasa kwa watu
wanaoishi mabondeni au kandokando ya mito.
Mikoa mingi nchini imepata adha ya mafuriko
kutokana na mvua zilizoanza kunyesha mwezi uliopita. Lakini kwa wakazi
wa vijiji vilivyopo kandokando ya Mto Rufiji, mvua zimewaletea wageni
hatari katika maeneo yao.
Wageni hawa ni viumbe hatari; ni mamba
waliowageuza wenyeji wao kuwa kitoweo na kuwafanya waishi kwa wasiwasi
wakihofia usalama wao.
Wakazi hawa wanashindwa kuendelea na maisha yao
kama kawaida, ikiwemo shughuli za kilimo ambazo huzifanyia ng’ambo au
pembezoni mwa mto huo.
Kwa muda mrefu sasa mnyama huyo amekuwa tishio kwa
wakazi wa Wilaya ya Rufiji. Wanyama hao wengi huishi katika mabwawa
yaliyopo katika Hifadhi ya Selous, lakini mvua inaponyesha na maji
kujaa mtoni, mamba hurahisishiwa kazi ya kuwinda binadamu.
Wakazi wa vijiji vya Utete, Chemchem, Mkongo,
Ngorongo, Nyaminywili, Mloka na Mwaseni hujishughulisha na kilimo cha
mazao ya mahindi, mpunga, ndizi na matikitimaji kando ya mto huo.
Wengi wao hulazimika kuvuka mto huo ili kwenda
ng’ambo ya pili kulima, au kuwinda ndege na usafiri wao mkubwa ni
mitumbwi ambayo siyo salama katika kipindi hiki.
Hivi karibuni, mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi
tawi la Lumumba katika kijiji cha Kilimani Mashariki, Saidi Simba (60)
aliliwa na mamba wakati akivuka mto huo.
Akiwa na mwanawe wa kiume, Seif Saidi (5) mtumbwi waliokuwa wakisafiria ulijaa maji na kumlazimu kushuka ili ayaondoe.
Aliposhuka tu alipokelewa na mamba ambaye
alimzamisha na kutoweka naye huku mtoto wake akibaki na taharuki na
kulazimika kupiga kelele kuomba msaada.
Ofisa mtendaji wa Kijiji cha Kilimani Mashariki,
Masudi Mminge anasema kuwa katika eneo hilo, mamba huweka makazi hasa
wakati wa mvua.
Anasema tatizo la wanyama hao ni kubwa katika kijiji chake na vijiji vya jirani, hasa katika kipindi cha masika.
0 comments:
Post a Comment