Sunday, May 11, 2014

Mbuyu Twite asubiriwa airport DR Congo 

 

Twite.  

UKIZUBAA umeachwa. Beki wa Yanga, Mbuyu Twite bado hajasaini mkataba mpya wa kuendelea kuichezea timu hiyo huku uongozi ukimhakikishia kumpa maslahi mazuri lakini kichwani ana akili nyingine kabisa kwani klabu za AS Vita na FC Lupopo zinamnyemelea.
Klabu hizo za DR Congo zinafuatilia kila kitu kuhusu Twite na Yanga na zinamsubiri akikanyaga ardhi ya nchi yao, mwenye kisu kikali anamaliza dili haraka.
Asili ya Twite ni DR Congo licha ya kuwa na uraia wa Rwanda.
Hapa nchini, viongozi wa Yanga wamemhakikishia Twite maslahi mazuri yatakayomfanya asiifikirie timu nyingine lakini bado inampiga danadana za siku ya kusaini mkataba mpya huku mwenyewe akitaka kwenda DR Congo.
Beki huyo anayemudu kucheza nafasi ya kiungo, inadaiwa hana raha kutokana na kutomaliziwa mambo yake huku siku zikizidi kwenda lakini anapozungumza anasema: “Safi tu hakuna tatizo.”
“Nimekuwa katika mazungumzo na viongozi wa Yanga, tumekubaliana karibu kila kitu. Kilichobaki ni kusaini tu, kila tunapopanga hakuna linalokamilika nimewaomba tiketi ya ndege niwahi nyumbani nikapumzike,” alisema Twite.
Rafiki wa karibu wa Twite amesema, beki huyo anachukizwa na kitendo cha Yanga kuchelewa kumpa mkataba na akipewa tiketi ya ndege kwenda DR Congo kuna uwezekano mkubwa wa kujiunga na kati ya klabu ya AS Vita au FC Lupopo.
“Twite anawaheshimu sana Yanga, lakini Vita na Lupopo wanamtaka na akipewa tiketi ya ndege tu ujue hawezi tena kurudi Yanga kama hajasaini mkataba,” alisema rafiki huyo.
Hadi sasa Yanga imewapoteza wachezaji wawili Didier Kavumbagu na Frank Domayo kwa kushindwa kuingia nao mikataba haraka baada ya awali kwisha.

0 comments:

Post a Comment

Designed by Adamu Mwanakatwe