Mbeya City: Simba imekula kwenu
Wachezaji wa timu ya Mbeya City. City imewaambia Simba kwamba wamebugi kwa wanachokifanya kwa straika wao, Saad Kipanga na kwamba wao hawamuachii kwani wana mkataba naye.
Mchezaji huyo alizungumza na Mwanaspoti na
kuihakikishia kwamba amezungumza kwa kina na matajiri wa Simba, lakini
hajataka kuliweka bayana suala hilo kwa uongozi wa Mbeya City.
Mwanaspoti linajua kwamba Simba inafanya mambo
yake kimyakimya na imejidhatiti kwamba lazima kijana huyo avae jezi
nyekundu msimu ujao.
Mbeya City imefura na kumtaja Kipanga kwamba bado
ana mkataba wa mwaka mmoja na nusu na kama Simba amewaeleza vinginevyo
wamechemka. Katibu Mkuu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe, alisema kuwa
uongozi wao bado haujapanga kuwauza wachezaji ingawa suala hilo
linawezekana endapo pande zote mbili zitakutana na kukubaliana na si
vinginevyo.
“Tumesikia, mchezaji tumemuuliza amekataa
kuzungumza na viongozi wa Simba, ila ukweli anaujua yeye kikubwa ni
kwamba hakuna mchezaji ambaye tumepanga kumuuza,” alisema Kimbe.
“Kipanga ana mkataba na sisi tena wa muda mrefu,
hivyo kama Simba wanafanya mazungumzo na mchezaji huyo ni kosa,
wanatakiwa kuja kuzungumza na viongozi ili wasikie sisi tunasemaje, huko
ni kuwarubuni wachezaji.”
Alisema kuwa Simba wanafahamu kanuni zote za
usajili ambazo wanatakiwa kuzifuata huku akisisitiza kuwa endapo Kipanga
angebakiza mkataba wa miezi sita ilikuwa ni ruhusu kufanya naye
mazungumzo.
“Sheria zipo wazi ambazo kila kiongozi wa soka
anazifahamu, Kipanga tulimsajili wakati wa usajili wa dirisha dogo,
wakiamua kuja ndipo tutajua cha kuwajibu zaidi na watajua mkataba wa
mchezaji huyo umebaki wa muda gani, ila napo wanaweza kumkosa kwani
hatuna mpango wa kumuuza kwa sasa,” alisema Kimbe.
Kiongozi Simba aonya
Mweka Hazina Msaidizi wa zamani wa Simba Humprey
Laban, ameuonya uongozi wa klabu hiyo kwamba usithubutu kusajili
wachezaji waliowahi kukipiga timu hiyo kisha kuhamia Yanga kwani endapo
utafanya hivyo utakuwa unakaribisha hujuma.
Simba iko kwenye mazungumzo na kipa Ally Mustapha
‘Barthez’ aliyemaliza mkataba na Yanga. Laban alisema kwa uzoefu wake
wachezaji waliowahi kuhama kutoka Simba kwenda Yanga kisha kurudi tena
ndio wamekuwa wakihusika katika kufanya hujuma.
“Simba chonde chonde wachezaji waliohamia Yanga
kutoka kwetu tusiwarudishe tena wengi wao ndio ambao wamekuwa wakihusika
katika kutuhujumu, tatizo ni kwamba wachezaji wa namna hii wanakuwa na
marafiki kutoka pande zote hivyo inakuwa rahisi sana wao kutumika kwenye
michezo michafu naomba waachane nao kabisa,” alisema.
0 comments:
Post a Comment