Aliyemuiba Domayo Yanga yupo hoi
YANGA wameanza mipango ya kuziba nafasi ya aliyekuwa kiungo wao
Frank Domayo aliyehamia Azam FC,lakini huku nyuma bosi aliyefanya zoezi
la kimafia kumsainisha nyota huyo ameugua.
Usajili wa Domayo ulianzia jijini Dar es Salaam
ambapo mjomba wa kiungo huyo alikutana na mabosi wa juu wa Azam na
kukubaliana kila kitu na hatimaye kuchukua fedha za malipo za ndugu
yake.
Baada ya hilo kukamilika ikaja kazi ya pili ya
nani atamsainisha mkataba Domayo aliyekuwa katika kambi ya Taifa Stars
iliyopo Tukuyu, Mbeya. Baada ya tathmini fupi kazi hiyo akapewa mtu
anayeitwa Jemedari Said Kazumali ambaye pia ni meneja wa kikosi
akiongozana na wenzake wanne wakatua Mbeya kwa ndege ya haraka.
Kama lilivyo jina lake Jemedari aliifanya kazi
hiyo na kiungo huyo akawa mali ya Azam ingawa baadae siku hiyo ilizuka
tafrani iliyosababisha atiwe kizuizini na Askari wa Jeshi la Polisi
ingawa hawakupelekwa kituoni.
Alipoachiwa na kurudi jijini Dar es Salaam baada
ya siku mbili akaanza kuugua ghafla ambapo alilazimika kukimbizwa
hospitali usiku ambapo alipumzishwa kutokana na hali yake katika
Zahanati ya Arafa iliyopo Gongo la Mboto.
“Nimepumzishwa tangu jana usiku baada ya hali
yangu kuwa mbaya sana, kikubwa ni malaria na tumbo, nilipofika hapa
hospitali madaktari hawakutaka kuniruhusu kurudi nyumbani kutokana na
hali yangu,” alisema Jemedari siku ya Jumamosi akiliambia Mwanaspoti.
Kidogo juzi hali ikabadilika ambapo Jemedari
alirudi nyumbani ingawa hali yake haijatengamaa. “Nimerudi nyumbani
lakini bado afya yangu haijaimarika sawasawa, sitaki kuhusisha kuumwa
kwangu na mambo mengine lakini nasisitiza nipo ngangari waambie wote,”
alisema Jemedari baada ya kuhisi kuna mkono wa mtu katika kuumwa kwake.
Wakati hali ikiwa hivyo kwake, mmoja wa mabosi wa
juu wa Azam ambaye naye alihusika katika usajili Domayo (jina tunalo)
naye alikuwa hoi kitandani nyumbani kwake akiugua mafua makali ambayo
inasemekana hayajawahi kumshika katika kipindi cha miaka miwili.
0 comments:
Post a Comment