Monday, May 5, 2014

 

Pep Guardiola. 


MANCHESTER, ENGLAND
KICHAPO ilichokishusha Real Madrid cha mabao 4-0 dhidi ya Bayern Munich uwanjani Allianz Arena Jumanne iliyopita, kimeibua jambo kuhusu hatima yao kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.
Mechi hiyo ilikuwa na taswira muhimu kwa makocha wawili mahiri wa Ulaya kuhusu hatima zao ya msimu ujao. Carlo Ancelotti wa Real Madrid na Pep Guardiola wa Bayern Munich, hii ni baada ya klabu ya Manchester United kusaka kocha mpya kwa sasa.
Kocha wa timu ya taifa ya Uholanzi, Louis van Gaal, ambaye atamalizana na timu hiyo baada ya fainali za Kombe la Dunia zitakazoanza mwezi ujao kule Brazil, ndiye anayepewa nafasi kubwa ya kuwa kocha mpya wa Man United baada ya kumtimua kocha, David Moyes, Aprili 22 ikiwa ni baada ya kudumu na klabu hiyo ya Old Trafford kwa miezi 10 tu.
Ukimweka kando Van Gaal ambaye mwanzoni ndiye aliyeonekana kuwa na nafasi ya kutua Man United, kuna makocha wengine ambao mabosi wa klabu hiyo wanaweza kufikiria kuwapa kazi baada ya matokeo ya mechi za nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kuhusu Guardiola
Baada ya kustaafu soka akiwa mchezaji mwaka 2006, Guardiola alihamia kwenye ukocha na kufanikiwa akiwa ametwaa mataji 14 ndani ya miaka minne aliyodumu na Barcelona kuanzia 2008 hadi 2012.
Kabla hajakabidhiwa kibarua cha kuinoa timu hiyo, Guardiola alitumikia mwaka mmoja akiwa kocha wa timu B ya Barcelona, ambapo aliweza kuiongoza vyema na kuwavutia mabosi wake kiasi cha kuamua kumpa kazi baada ya Frank Rijkaard kuondoka.
Kwa sasa yupo na Bayern Munich, lakini kipigo kutoka kwa Real Madrid kimeibua hofu kubwa katika uhai wa maisha yake kwenye klabu hiyo ya Ujerumani. Guardiola mambo yake yanaonekana kutokuwa mazuri Bayern kutokana na mabosi wa timu hiyo na wachezaji waliowahi kung’ara na kikosi hicho kuushambulia mtindo wa soka lake, wengi wakimshutumu kwamba amekwenda kuiharibu timu hiyo. Man United inaweza kubadili kibao na kuhamia kwa kocha Guardiola.
Sir Alex Ferguson, ambaye aliongoza Man United kwa miaka 26 kabla hajamchagua Moyes kuwa mrithi wake mwaka jana, alikutana na Guardiola mjini New York, Marekani wakati kocha huyo alipochukua mapumziko ya mwaka mzima nje ya soka.
Aprili mwaka jana, kocha huyo Mhispaniola alisema hakufahamu vizuri kama chakula cha usiku alichokula na Ferguson kilikuwa na dhamira ya kumshawishi awe mrithi wake Old Trafford. Baadaye Guardiola alichagua kwenye Bayern na hapo Ferguson akaamua kumchagua Moyes kuwa mrithi wake.
Ferguson alikuwa na imani kuhusu Guardiola baada ya kushindwa dhidi yake kwenye fainali mbili za Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2009 na 2011.

0 comments:

Post a Comment

Designed by Adamu Mwanakatwe