Ukawa nusura ‘wamchenjie’ Mbowe
Mwenyekiti wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Freeman Mbowe (kulia) na Mjumbe wa Umoja huo, James Mbatia wakiingia katika Ukumbi wa African Dream mjini Dodoma walipohudhuria mkutano wa wajumbe wa Bunge la Katiba wa umoja huo ambao wamegoma kuendelea kuhudhuria vikao vya Bunge. Picha na Edwin Mjwahuzi
Dodoma. Wajumbe wa Mkutano wa Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa), juzi nusura wamgeuzie kibao mwenyekiti wao, Freeman Mbowe baada
ya kuchelewa kufika kwenye mkutano ulioandaliwa ikiwa ni siku moja
baada ya kususia kikao cha Bunge la Katiba.
Ukawa walikutana kwenye Ukumbi wa African Dream kwa ajili ya kujipanga baada ya kususia mkutano wa Bunge.
Mkutano huo ulioanza saa 4:18 ukiongozwa na
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba baadaye wajumbe walianza
kuhoji walipo viongozi wao, Freeman Mbowe na James Mbatia.
Mmoja wa wajumbe wa mkutano huo, Profesa Abdallah
Safari alisimama na kuhoji walipo viongozi hao hatua iliyoanza
minong’ono miongoni mwa wajumbe wakiwa na hisia kwamba huenda
wamewageuka na kwenda kwenye Kikao cha Kamati ya Uongozi.
“Tujue kabisa kama wametugeuka...Tumeshakubaliana
hakuna mtu kwenda kwenye Mkutano wa Kamati ya Uongozi, sasa kama
amekwenda tujue,” ilisikika sauti ya mmoja wa wajumbe.
Kuona hivyo, ilibidi Profesa Lipumba aanze
kuwapigia simu huku wajumbe wakiwa kimya kusikiliza nini kitafuata.
Baadaye Profesa Lipumba aliwaambia wajumbe kuwa ameongea nao wote na
wako njiani wanakuja.
Baada kusikiliza taarifa hiyo, wajumbe walianza
kutoa hoja mbalimbali. Saa 5:07 waliwasili Mbowe na Mbatia kwa pamoja na
kwenda kukaa kwenye nafasi zao mbele.
Mbowe baada ya kukaribishwa alisema: “Jamani
naomba radhi kwa kuchelewa, nilipigiwa simu na Katibu wa Bunge, John
Joel kuwa nahitajika kwenye kikao cha Kamati ya Bajeti...Nilikwenda kule
kwa kuwa nilijua masuala ya bajeti ni ya kitaifa.
“Lakini nilipofika, nikakutana na Kamati ya
Uongozi ya Bunge Maalumu la Katiba, nikawaeleza kuwa siwezi kukaa kwenye
kikao hiki, ingekuwa bajeti kama nilivyoelezwa sawa lakini hii
nawaambia sitashiriki,” alisema Mbowe na kushangiliwa.
Baada ya hapo, Mbowe alieleza msimamo wa Ukawa
kuwa hautashiriki Bunge la Katiba hadi hapo utaratibu utakapobadilishwa
wa mwenendo wa Bunge la Katiba.
Hata hivyo, baadaye Mbowe aliwatoa nje waandishi wa habari akisema wawapishe kwa ajili ya kuzungumza mambo yao ya jikoni.
0 comments:
Post a Comment