Rais Kikwete aombwa kufuta hati shamba la mwekezaji
Rais Jakaya Kikwete ameombwa kufuta hati miliki ya sehemu ya eneo la
mwekezaji wa kampuni ya Susumua Holdings ambalo ameshindwa kuliendeleza
ili kuligawa kwa wananchi ambao hawana ardhi kwa ajili ya kilimo na
ufugaji.
Ombi hilo lilitolewa na wananchi wa kijiji cha Kwamsisi, wilayani
Handeni, wakati wa mkutano wa kijiji hicho uliokuwa ukizungumzia mgogoro
uliopo baina ya mwekezaji wa kigeni na wananchi hao.
Walisema wanamuomba Rais Kikwete kuingilia kati mgogoro huo kwa kuligawa
eneo ambalo mwekezaji amelihodhi bila ya kuliendeleza huku wakazi wa
kijiji hicho wakiwa hawana sehemu ya kuendesha shughuli zao za kilimo na
ufugaji.
Walidai mwekezaji huyo kwa sasa analima eneo dogo kwa ajili ya mazao
huku akiacha karibu robo tatu ya shamba bila ya kuliendeleza kwa
kipindi kirefu jambo linalowafanya kuona hawatendewi haki na kuitaka
serikali kufuta hati miliki ya sehemu iliyobaki.
"Tunataka ardhi hiyo igawiwe upya kwa wananchi kwani mwekezaji amekuwa
akitukandamiza sisi wananchi kwa kujua tupo kijijini hapa akidhani
hatuna uwezo wa akili kitu ambacho hatutakubali "alisema Makame
Mwinyiheri.
Nae Afisa Mtendaji kata wa kijiji cha Kwedikwazu, Idrisa Nassor alisema
mwekezaji huyo kila mara amekuwa akijiongezea eneo kwani awali alikuwa
anamiliki ekari 6,174 na sasa amefikisha ekari 7,295.
“Tuna kaya zaidi ya 200 zinaishi ndani ya eneo lake ambazo zinakosa
huduma muhimu hivyo tunaomba shamba lipunguzwe kwa ajili ya maslahi ya
wananchi kuliko kutoa kwa wawekezaji wanao tuumiza ambao
wanatusababishia kukosa huduma muhimu za kijamii" alisema Nassor.
Akizungungumzia malalamiko hayo ya wananchi, mwekezaji wa shamba hilo,
Rony Nightngali alisema eneo hilo alimilikishwa kihalali na serikali kwa
ajili ya kuendesha kilimo cha matunda na mbogamboga, lakini uwelewa
mdogo wa masuala ya haki za umiliki wa ardhi kwa wanakijiji hao ndiyo
unapelekea migogoro ya mara kwa mara .
Alisema kampuni yake imeamua kuwekeza karibu na maeneo ya kijiji hicho
ili kutoa fursa za ajira kwa wananchi pamoja na kukuza pato la uchumi
wao kutoka na kushiriki katika ulimaji wa mazao.
0 comments:
Post a Comment