Rais Jakaya Kikwete akiwa katika mahojiano maalumu na Mtangazaji Daniel Kalinaki wa Kituo cha Televisheni cha Nation (NTV) kinachomilikiwa na Nation Media Group, Ikulu jijini Dar es Salaam. Picha na Ikulu
Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete ameendelea kusisitiza kuwa
Tume ya Jaji Joseph Warioba haina ushahidi kwamba Watanzania wengi
wanataka muundo wa Muungano wa serikali tatu.
Kauli hiyo aliitoa wiki hii jijini Dar es Salaam
kwenye mahojiano maalumu na Kituo cha Televisheni cha NTV kilichopo
chini ya Nation Media Group (NMG).
Baadhi ya vyombo vingine vya habari vilivyo chini
ya NMG ni gazeti hili la Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti kwa upande
wa Tanzania, Daily Monitor kwa upande wa Uganda na Daily Nation kwa
upande wa Kenya.
Rais Kikwete ambaye moja ya mambo atakayokumbukwa
kwenye uongozi wake ni kuasisi mchakato wa Katiba, alizungumzia hoja ya
serikali tatu akisema, hakuna ushahidi kwamba Watanzania wengi wanataka
muundo wa Muungano wa serikali tatu.
“Hakuna ushahidi kwamba watu wengi katika nchi hii
wanataka serikali tatu, hakuna ushahidi wa namna hiyo, hata tume
yenyewe haikubaini hicho. Kinachofanywa na vyombo vya habari ni kuandika
habari za wajumbe wa Bunge la Katiba wanaotaka serikali tatu, ndiyo
kwenye masilahi yao, wanapaza sauti za wale wanaotaka serikali tatu, hao
ndiyo sauti zao zinasikika. Lakini hawataki kupaza sauti za wale
wanaotaka serikali mbili,” alifafanua.
Hii ni mara ya pili kwa Rais Kikwete kuikosoa
ripoti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph
Warioba. Mara ya kwanza aliikosoa wakati akizindua Bunge la Katiba Machi
21 mjini Dodoma.
Rais Kikwete ambaye amewahi kuwa Waziri wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa kipindi cha miaka 10, katika
mahojiano hayo alisema katika kuadhimisha miaka 50 ya Muungano, jambo
muhimu na kubwa ni kuendelea kuwapo kwa Muungano.
“Tunayo mifano ya nchi zilizojaribu kuungana, lakini zilishindwa, Senegal-Gambia, Ghana-Guinea, Misri na Libya.
“Muungano umeendelea kuwepo kwa nusu ya karne ni
mafanikio makubwa. Kumekuwepo na wakati mgumu na changamoto mbalimbali,
lakini tumeweza kukabiliana nazo na umeendelea kuwa imara zaidi. Siyo
kuendelea kuwepo tu pia umeendelea kuimarika na mchakato wa mabadiliko
ya Katiba utaimarisha zaidi Muungano na tutakuwa na Muungano imara baada
ya kupata Katiba Mpya,” alifafanua Rais Kikwete.
Akizungumza kwa kujiamini kutokana na uzoefu wake
wa muda mrefu ndani ya CCM na Serikali, Rais Kikwete alisema Muungano
ulikotoka ulikuwa imara na umeendelea kukua katika hali ya uimara wake.
“Kuna mambo ambayo tumefanya yamezidi kuimarisha Muungano na umeendelea kuwa na mafanikio makubwa.”
Alisema suala si kuendelea kwa muundo ulivyo sasa,
suala la msingi ni kujadili namna ya kutengeneza muundo wa Muungano,
kwamba upi ni bora.
0 comments:
Post a Comment