Mtikila ‘apiga hela’ mkutano wa Ukawa
Dodoma. Kiongozi wa Chama cha DP, Mchungaji Christopher Mtikila,
juzi alitoa mpya ya aina yake katika Mkutano wa Umoja wa Katiba ya
Watanzania (Ukawa) pale alipopigia debe kitabu chake ambacho
kilinunuliwa kwa idadi kubwa na wajumbe wenzake.
Kundi la Ukawa lilikuwa na mkutano wake wa kuweka
mikakati kwenye Hoteli ya African Dreamer ikiwa ni siku moja baada ya
kutoka nje ya Ukumbi wa Bunge Maalumu la Katiba linaloendelea mjini
Dodoma.
Katika mkutano huo, Mchungaji Mtikila alikuwa mtu
wa tano kuzungumza na sehemu kubwa ya hotuba yake ilikuwa ikiwalalamikia
wajumbe wa CCM kuwa hawana nia ya kutengeneza Katiba na kazi yao ni
kuwazomea na kushangilia hata anayeongea pumba.
Mtikila alisema kuwa wao kama Ukawa wanaona kwa
hali iliyopo hakuna Katiba inayoweza kupatikana. “Kwa mazingira haya,
hakuna Katiba itakayopatikana na kukubalika duniani, haipo,” alisema
Mtikila.
Kabla ya kuhitimisha, Mtikila alitumia nafasi hiyo
kutangaza kuwa ana kitabu kilichokuwa kikizungumzia hoja yake
iliyokataliwa na Mwenyekiti wa Bunge ya kwanini mchakato wa Katiba
usivunjwe.
“Halafu ndugu mwenyekiti, mimi nina kakitabu
kangu, kadogo tu tumefanya kazi juzi na jana kukiandaa. Tulioshirikiana
nao sasa wanataka kuja Dodoma kwa mguu, sasa kakitabu haka kako hapa,
mnichangie. Nimechelewa nilikuwa kwa wale wachapaji,” alisema na
kuongeza:
“Ni mambo ambayo Mheshimiwa Sitta aliwaambia
waandishi wa habari nimenyimwa nafasi ya kutoa hoja binafsi kwa sababu
nimegawa uchochezi kwa hiyo uko humo na ulipofika kwa wananchi, unafanya
kazi takatifu kabisa...Hivi sasa niko kwenye kompyuta natengeneza kitu
kizuri zaidi,” alisema Mtikila.
Baada ya kauli hiyo, wajumbe walianza kumiminika alipokuwa amekaa na kununua kama njugu vitabu hiyo vyenye kurasa 40.
0 comments:
Post a Comment