Mbowe: Hakuna aliyemtusi Mwalimu Nyerere, wala anayetaka kuvunja Muungano
Mwenyekiti wa Umoja wa Katiba ya Watanzania (Ukawa), Freeman
Mbowe, amesema uamuzi wao wa kutoka nje ya Ukumbi wa Bunge ni sahihi kwa
kuwa ni njia ambayo imeonekana kwao kuwa inafaa kudai haki ya
Watanzania wote.
Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa Kambi ya Upinzani
Bungeni, alisema hayo muda mfupi baada ya kumalizika kwa mkutano wa
ndani wa Ukawa.
Mkutano huo pamoja na mambo mengine ulijadili
mikakati mbalimbali inayohusu umoja huo ambao sasa wanapeleka masuala
yao kuhusu mchakato wa Katiba Mpya kwa wananchi.
Ukawa pamoja na baadhi ya wajumbe wa Bunge la
Katiba kutoka kundi la 201, walitoka nje ya Ukumbi wa Bunge mjini
wakidai kutoridhishwa na mwenendo wa Bunge hilo lenye lengo la
kutengeneza Katiba Mpya.
“Kuendelea kushiriki mchakato huu, ni kuubariki na
kuupa uhalali udhalimu unaoendelea ndani ya Bunge Maalumu, hatuwezi
kushiriki mjadala wenye matusi, kejeli, dharau na unaopotosha umma, kwa
kupindisha kauli zilizowahi kutolewa na viongozi wetu,’ anaeleza Mbowe.
Mbowe anasema wajumbe wa upande wao kila walipotoa
mtazamo wao, wakieleza ukweli, wajumbe wa upande wa pili wanapopata
nafasi ya kuchangia mjadala badala ya kutoa mapendekezo yao na kuyatetea
kwa hoja, wanageuza ukweli wa maoni yaliyotolewa na wale wa upande wa
Ukawa, anasema ni karaha ambayo ni vigumu kuielezea ikaeleweka.
Akahoji wanaodai wamekosea kujitoa katika mijadala
hiyo ikiwa wanafurahishwa na udhalilishaji ambao wamefanyiwa tangu
kuanza mjadala unaohusu sura ya kwanza na sita za Rasimu ya Pili ya
Katiba Mpya.
Anataka pia watu wajiulize, je kwa mchakato wa
aina hii kitapatikana kile wanachotaka? Anasema kazi yao kama vyama vya
siasa ni kuweka shinikizo na kujenga hoja zenye kushinikiza kupatikana
kile kinachohitajika kwa masilahi ya taifa.
Anasema hawawezi kuwa sehemu ya mijadala
inayopuuza maoni ya wananchi ambayo yamepatikana kwa kukusanywa na
chombo (Tume ya Mabadiliko ya Katiba) kilichoundwa na serikali na
kufanya kazi kwa mujibu wa sheria iliyoidhinishwa na Bunge la Jamhuri ya
Muungano.
Mbowe anabainisha kuwa baada ya kubaini kutokuwapo
uwezekano wa kubadili nyendo za wenzao bungeni, wakaafikiana kuwa
kinachofuata ni kuunda busara yoyote ambayo wanaweza kuitumia kuokoa
taifa dhidi ya genge la watu kama wale, ambao wamekaririshwa maneno.
“Wao wanatulaumu Ukawa tunaweka misimamo, lakini
wao wanakuja na mambo ambayo wameyajadili katika mikutano yao ya ndani
na Waziri Mkuu akiwa miongoni mwao. Wanaweka mikakati ya kuzomea, watu
wanazomewa pale, kauli za utenganisho zinatajwa na watu wanashangilia
bila kujali kuwa wanapasua taifa - hatuwezi kuendelea kuwa sehemu ya
wapasua taifa,” anasema Mbowe.
Anasema wameamua kwenda kwa wananchi kuwaambia
kinachoendelea bungeni, wao ndiyo wataamua anasema kadhalika waliobaki
siku za usoni wanaweza wakapata busara wakaona kuwa kutunga Katiba peke
yao ni jambo lisilo na uhalali.
0 comments:
Post a Comment