Friday, April 18, 2014

Moyes abakiza siku chache za kumpisha Jurgen Klopp

 

Kocha David Moyes


KAMA David Moyes angetilia shaka uteuzi wake wa kuwa kocha mpya wa Manchester United kwenye miezi ya mwanzoni tu hadi kufika sasa angekuwa na ufahamu wa nyakati mbaya zinazoikumba klabu hiyo kwa sasa.
Mbaya zaidi alirithi timu ambayo imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu na pia alikuwa na pesa za kutumia kufanya usajili wa nyota anayemtaka. Wapi palikwenda kombo?
Kwa msimu wake wa kwanza kushindwa kutetea ubingwa lisingekuwa jambo baya sana, lakini si kushindwa kuwamo kwenye nne bora. Man United haijawahi kumaliza msimu ikiwa nje ya tatu bora tangu 1991.
Tazama timu kama Everton na Tottenham Hotspur inapigana vikumbo na Man United kwenye kugombea nafasi ya sita na saba. Hii ni aibu kwa timu ambayo ina pesa za kutosha za kufanya usajili wa wachezaji inaowataka. Ni aibu pia kwa klabu kubwa yenye hadhi kubwa kama ilivyo Man United.
Jumapili hii, Man United itakwenda Goodison Park kumenyana na Everton kwenye Ligi Kuu England. Kipigo kwenye mchezo huo kitazima rasmi ndoto za Man United za walau kumaliza nafasi ya nne ili kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Kwa msimu huu, timu yoyote itakayofanikiwa kutwaa ubingwa, iwe Chelsea, Manchester City au Liverpool, basi shabiki wa Man United atakuwa na swali gumu sana kwa Moyes.
Mashabiki wake wa zamani katika klabu ya Everton walishamtabiria kwamba atafukuzwa kazi Old Trafford. Kwa jinsi ambavyo msimu huu umekwenda ni ngumu kuamini kama Mskochi huyo ataendelea kubaki kwenye kibarua hicho msimu ujao.
Jurgen Klopp atajwa kuwa mrithi
Gazeti la Daily Mirror limefichua kwamba mabosi wa Man United kwa sasa wanamfukuzia kocha Jurgen Klopp na kuamini atakuwa mwafaka wa kumrithi Moyes kwenye klabu hiyo. Kuna kila dalili za Moyes kusitishiwa ajira yake mwisho wa msimu.
Gazeti hilo la Mirror liliripoti: “United inaamini mtindo wa soka la Klopp na mbinu zake za ukocha kitu kinachohitajika sana kwenye klabu hiyo baada ya Moyes kutibua mambo katika msimu wake wa kwanza.”
Kwenye mchakato huo, Man United pia inahusishwa na mpango wa kumchukua Mdachi Louis van Gaal. Lakini, mashabiki wa Man United wanaonekana kufarijika zaidi na kocha Klopp.
Sawa, ni mapema sana kutamka kwamba uteuzi wa Moyes lilikuwa kosa kubwa. Lakini, bodi ya klabu ya Man United inafikiria moja ya majina hayo mawili, Klopp na Van Gaal kumrithi Moyes huku Klopp akionekana kupata sapoti kubwa ya mashabiki wengi kwenye mchakato wa kupatiwa kibarua hicho.
Man United itasajili nyota inayemtaka.

 

0 comments:

Post a Comment

Designed by Adamu Mwanakatwe