Al Ahly wambakiza Cannavaro Cairo
Nadir Haroub ‘Cannavaro’
AL AHLY haijaamini kwamba imewang’oa Yanga kwenye Ligi ya
Mabingwa Afrika. Lakini baada ya kutimiza azma hiyo, itafanya usajili wa
wachezaji wawili wapya muhimu.
Nyota hao itakaowanunua ni kiungo na beki safu ambazo zina utata mkubwa kwenye kikosi chao.
Jopo la usajili la Ahly limemtaja, beki kisiki wa
Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kama mlengwa wao namba moja na
wamemfanyia utafiti wa kina kwenye mechi zote mbili walizocheza na Yanga
na watawasilisha maombi yao rasmi Jangwani kwavile wamevutiwa na uwezo
wa mchezaji huyo kwenye kuzuia, kufunga na kuhamasisha.
Jana Jumatatu walikuwa na kikao kirefu na baada ya
mazoezi ya jioni walitarajia kufikia muafaka na kuwasilisha maombi
Yanga kabla ya haijakwea pipa usiku wa leo Jumanne na kuwasili Dar es
Salaam kesho Jumatano alfajiri.
Mmoja wa viongozi wa Ahly aliyejitambulisha kwa
jina la Mohammed Saed alisema tangu awali lengo lao ilikuwa ni kusajili
beki na kiungo kama wangefanikiwa kuiondosha Yanga, lakini baada ya
kukamilisha azma hiyo wanarudi mezani kuandaa utaratibu wa kuishawishi
Yanga iwape mchezaji huyo aliyewafunga bao pekee la jijini Dar es
Salaam.
Mohammed alisema wamepokea mapendekezo kutoka
katika benchi lao la ufundi ambalo limemtaja moja kwa moja beki huyo
huku wakimfikiria kiungo mmoja wa Yanga ambaye hakumtaja kwa madai kuwa
wanasubiri ripoti nyingine ya benchi la ufundi kuhusiana na nafasi hiyo
na ufanisi wa viungo wa Yanga kwenye mechi ya marudiano.
“Kuna nafasi ambazo tunatakiwa kuzifanyia
maboresho yule beki wa Yanga anayevaa jezi namba 23 (Cannavaro)
tunamhitaji lakini pia kuna kiungo mmoja ambaye tunasubiri tathmini ya
kocha kwenye mechi ya marudiano tufanye uamuzi,”alisema Mohammed ambaye
amekuwa mstari wa mbele kwenye mechi zote mbili za Dar es Salaam na
Alexabdria.
Katika mazoezi ya mwisho ya Yanga kwenye Uwanja wa
Max mjini Alexandria, mmoja wa wapiga picha wa televisheni ya timu hiyo
alipewa kazi maalum ya kuchukua picha za Cannavaro tu wakati akijifua
ambapo alikuwa akimfuatilia kwa karibu zaidi kuliko mchezaji yeyote.
Kocha msaidizi wa Ahly, Ahmed Ayoub alizungumza na
Mwanaspoti jana Jumatatu na kukiri kumtaka beki huyo lakini akasisitiza
kuwa uongozi wa juu ndio wenye mamlaka ya kutoa tamko kwavile wao kazi
yao ni kupendekeza.
Yanga yazindua jezi
Katika mechi mbili dhidi ya Ahly, Yanga ilitumia
jezi mpya za aina mbili ambazo ilithibitisha kwamba zimenunuliwa
Uingereza. Jijini Dar es Salaam ilitumia jezi mpya zilizokuwa na
mistari ya njano na kijani ambazo hawakuwahi kuzitumia miaka ya
karibuni.
Katika mchezo wa marudiano juzi Jumapili uliopigwa
mjini Alexandria, Misri walitambulisha uzi mwingine mpya ambao hauna
tofauti kubwa na jezi za timu ya taifa ya Brazil
0 comments:
Post a Comment