OVYO: Moyes akiri hali ni mbaya Old Trafford
MANCHESTER, ENGLAND
HALI ni mbaya zaidi. Mtu anayesakamwa zaidi katika
mchezo wa soka kwa sasa, kocha David Moyes wa Manchester United,
amekiri kuwa hali ni mbaya sana Old Trafford kuliko wakati mwingine
wowote.
Wakati mashabiki wa timu hiyo wakiamini kuwa timu
yao ilikuwa imeshinda 2-1 katika pambano dhidi ya Fulham juzi Jumapili,
katika sekunde za majeruhi, mshambuliaji wa Fulham, Darren Bent,
alifunga bao lililoipatia sare ya 2-2 timu yake katika dimba la Old
Trafford.
Bao hilo limeiacha Manchester United ikiwa pointi
tisa nyuma ya timu inayoshika nafasi ya nne, Liverpool, ambayo saa 24
kabla ya mechi hiyo ilikuwa imeiburuta Arsenal mabao 5-1 katika Uwanja
wa Anfield.
Alipoulizwa kama alijua kuwa mambo yangekuwa kama
yalivyo sasa, Moyes alijibu: “Hapana kwa kweli. Imekuwa kama hivi msimu
huu, lakini leo (juzi Jumapili) imekuwa mbaya mno. Unaweza kusema kwamba
tulikuwa laini sana akilini na hatukumaliza kazi yetu. Nakubali.
“Tulitawala mchezo. Kufungwa bao moja lilikuwa jambo baya. Kiasi
cha nafasi tulizotengeneza, tulizojaribu na jinsi tulivyocheza
ilishangaza sana kwa nini hatukushinda, yaani sielewi.
“Tulimiliki mpira kadiri tulivyoweza. Tungeweza
kufunga zaidi. Wachezaji walijaribu na mabao yalikuja, hata wakati
walipofungwa 2-1 na dakika tano kuongezwa Fulham bado hawakucheza
vizuri, walituacha sana na mpira kwa hiyo lilikuwa suala la kupoteza
muda, lakini ghafla tukawapa bao la kijinga sana.
“Wachezaji wameumia sana. Naona kila siku jinsi
wanavyoumizwa kwa sababu matokeo hayaji kama wanavyotaka. Lakini tuna
timu nzuri na kuna timu chache sana zinazotamani kucheza na sisi, nina
uhakika.”
Kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi,
Manchester United sasa iko katika hatari ya kukosa nafasi ya kucheza
Ligi ya Mabingwa Ulaya na Moyes alipoulizwa kuhusu suala hilo, alijibu
kwa kifupi: “Tutajaribu kadiri tuwezavyo.”
Beki wa zamani wa Liverpool, Jamie Carragher,
ambaye kwa sasa ni mchambuzi mahiri wa soka England, alikiri kwamba
hajawahi kuona timu inajihami kwa kiasi kile kama ambavyo Fulham
ilifanya katika mechi dhidi ya Manchester United.
0 comments:
Post a Comment