Thursday, August 13, 2015

WAMEDATISHWA au wamekurupuka? Ndivyo unavyoweza kuhoji kutokana na kasi waliyonayo wasanii katika kuchangamkia siasa wakijitosa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.

Wasanii wa uigizaji, waimbaji na wengine wameuchangamkia Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu wa 2015 na baadhi yao wamepenya kwenye kura za maoni na wengine kwenda na maji baada ya kukatwa.
Irene Uwoya alifanikiwa kupenya kupitia CCM viti Maalumu Vijana Mkoa wa Tabora, Mohammed Mwikongi ‘Frank’ yeye amepeta kupitia ACT, Joseph Haule ‘Prof Jay’ na Afande Sele wamepenya mkoani Morogoro kupitia vyama vya Chadema na ACT, Keysher, Said Fella walipeta kupitia CCM.
Fella alikuwa akiwania udiwani, wakati Keysher alipenya kwenye ubunge viti maalumu walemavu mjini Dodoma.
Wema Sepetu, Wastara Juma, Steven Mengele ‘Steve Nyerere’, Juma Chikoka ‘Chopa Mchopanga’ ni baadhi ya waliopigwa chini kupitia chama cha CCM, Rashid Mwinshehe ‘Kingwendu’ yeye bado haijafahamika kama kapenya kupitia CUF au la.
Sugu
Safari hii kumekuwa na mwamko mkubwa kwa baadhi ya wasanii kujitokeza kujaribu bahati zao ikiwa ni mara ya kwanza kwa wasanii wa filamu kuchukua uamuzi mzito kuomba ridhaa kwa raia, watu wa muziki wao tayari wapo Bungeni.
Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, Vicky Kamata, Martha Mlata ni baadhi ya wasanii wa muziki waliofungua pazia la wasanii kutwaa viti vya ubunge tangu walipojitosa katika uchaguzi uliopita.
Kabla ya hapo alikuwapo marehemu Kapteni John Komba na kushinda kwa Sugu kunaelezwa kama ndiyo sababu iliyowaamsha wengine, kwani walihisi kumbe kila kitu kinawezekana kwa kuwa haikutarajiwa kama Sugu angepita kupitia upinzani na safari hii ameteuliwa tena kutetea nafasi yake.
Mwaka huu, wasanii wa filamu ‘Bongo Movie’ waliamua kujaribu bahati zao na kujitokeza kuomba ridhaa ya kuwa wabunge kupitia vyama va kisiasa huku wasanii wengi wakiomba kupitia CCM na wawili tu wakiomba kupitia vyama vya upinzani.
Frank ameomba ridhaa ya kupeperusha bendera kupitia chama kipya cha ACT na anagombea jimbo la Segerea, huku mchekeshaji Kingwendu’akigombea jimbo la Kisarawe kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF).
Walioomba kupitia CCM walikuwa ni wengi na kura hazikutosha hivyo walishindwa na wakongwe wa chama hicho na kufanya watu waamini kuwa kupata nafasi ndani ya chama hicho si kazi rahisi, pamoja na wasanii kuwa na mvuto katika kukusanya watu, ila suala la kura za maoni ni changamoto.

0 comments:

Post a Comment

Designed by Adamu Mwanakatwe