
KELELE za mashabiki wa Yanga juu ya nani acheze na nani akae benchi katika kikosi chao, zinaonekana kuwaamsha wachezaji wa Simba ambapo sasa vita kali imeibuka katika nafasi tano tofauti uwanjani juu ya nani acheze na nani akae benchi.
Simba inaendelea na mazoezi yake mjini hapa kwa
wiki ya pili sasa ambapo uchunguzi wa Mwanaspoti umebaini kuwa nafasi
tano zinaonekana kuwa ngumu zaidi kucheza katika kikosi hicho.
Vita ya kwanza ipo katika nafasi ya beki wa kati
ambapo ina nyota watatu wenye uwezo unaolingana. Nyota hao ni Juuko
Murshid, Nahodha Hassan Isihaka na ingizo jipya Mohammed Faki.
Nafasi hii inaonekana kuwa ngumu kutokana na nyota
wote watatu kuwa na uwezo wa juu. Ujio wa Faki unaonekana kuwa tishio
zaidi kwa Isihaka kwani mwenzake ana utulivu mkubwa anapokuwa na mpira,
pia ni makini katika kufuata maelekezo ya kocha.
Lakini kazi haitakuwa rahisi kwa Faki pia. Juuko ni mtu wa kazi, hivyo nafasi yake ni kama ipo wazi kikosini hapo.
Kwenye beki ya kushoto kutakuwa na kibarua kizito
kutokana na nyota mpya wa timu hiyo, Samir Haji Nuhu kuonekana kuimarika
kila siku wakati ambapo chipukizi Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ akiwa
na majeraha. Uwezo ulioonyeshwa na Tshabalala msimu uliopita ni dhahiri
kuwa unaifanya nafasi hiyo kuwa ngumu pia.
Vita nyingine ipo katika eneo la kiungo ambapo
kama kocha Dylan Kerr atakuwa akitumia mfumo wa viungo wawili ni dhahiri
kuwa vita hiyo itakuwa kubwa kati ya Jonas Mkude, Awadhi Juma, Abdi
Banda na Said Ndemla.
Awadhi hakuwa na nafasi katika kikosi cha kwanza
msimu uliopita, lakini kwa sasa anaonekana kukubalika na Kerr hadi
kupewa cheo cha Nahodha Msaidizi wa muda. Kerr pia amekuwa akivutiwa na
jitihada zake uwanjani.
Mkude ndiyo kwanza alianza mazoezi jana Jumatatu wakati Ndemla bado hayuko fiti asilimia 100. Banda hajajiunga na wenzake bado.
Nafasi ya winga ya kushoto inaonekana pia kuwa
ngumu kutokana na uwepo wa Simon Sserunkuma, Mussa Hassan ‘Mgosi’ na
Peter Mwalyanzi ambapo wote ni wazuri. Mgosi anaweza pia kucheza straika
wa kati lakini usajili wa Laudit Mavugo kutoka Vital’O ya Burundi,
Hamis Kiiza na uwepo wa Ibrahim Ajibu na Elius Maguli unaonekana kuwa
sumu kwake.
Nafasi hiyo ya straika ndiyo ngumu zaidi kwa Kerr
kuchagua kutokana na nyota wote kuwa na uwezo wa juu licha ya kuzidiana
machache.
Kiiza ni mzuri kwa ufungaji lakini anahitaji
kucheza na mtu shapu pembeni kama Ajibu. Mavugo bado hajaonyesha vitu
vyake lakini mabao 34 aliyofunga Ligi Kuu Burundi yanatosha kuelezea
uwezo wake.
0 comments:
Post a Comment