


MACHI 26, mwaka huu ilikuwa ni siku ya kumi tangu msanii wa filamu Bongo, Kajala Masanja (pichani) asote rumande kwa kosa la kutakatisha fedha haramu, lakini afya yake ilitia simanzi.
Siku hiyo Kajala alifikishwa katika Makahama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu jijini Dar na kuonekana akiwa amepukutika tofauti na ubonge wake uliozoeleka.

Msanii huyo aliumia zaidi baada ya kunyimwa dhamana na hivyo kumwaga machozi mbele za watu.
Kajala ameunganishwa na mumewe Augustino Faraji baada ya kudaiwa kuuza nyumba iliyokuwa chini ya kizuizi cha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wakati akijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Akiwa kizimbani, msanii huyo alisomewa mashitaka na Mwendesha Mashitaka wa Mahakama hiyo, Reuben Swai ambaye alisema mnamo Aprili 14, mwaka 2010, Kajala na mumewe Agustino Faraji walimuuzia Emiliani Rugalila nyumba iliyopo Mbezi Salasala jijini Dar iliyowekewa kizuizi na Takukuru wakati wakijua kufanya hivyo ni kosa.

Hakimu Fimbo aliahirisha kesi hiyo mpaka Aprili 4, mwaka huu, huku akitaka mshtakiwa namba moja ahudhurie kesi hiyo.
Kajala na baadhi ya ndugu zake waliofurika kusikiliza kesi hiyo waliangua vilio baada ya hakimu huyo kusema kuwa dhamana bado imefungwa na mtuhumiwa kutakiwa kurejea tena rumande.
0 comments:
Post a Comment