ACHANA na mambo ya ushabiki, kama utaangalia rekodi za Kocha Patrick Phiri wa Simba na Marcio Maximo wa Yanga, inaonyesha hata kidogo Maximo hawezi kumkaribia Mzambia huyo.
Mambo matatu, uzoefu wa soka la Bongo, kufundisha timu za taifa au kimataifa na rekodi za kufundisha katika Bara la Afrika, vinaonyesha kumbeba juu Phiri kitakwimu dhidi ya Mbrazili huyo.
Phiri au Big Phiri anaonekana kuwa na uzoefu mkubwa ukilinganisha na Maximo ambaye kama ni kwa soka la Afrika, basi ameifundisha Taifa Stars pekee tangu mwaka 2006 hadi 2010 alipoondoka.
Lakini Phiri ambaye amezaliwa Afrika, analijua vema soka la barani hapa, pia ana uzoefu na rekodi zake ziko juu ukilinganisha na zile za Maximo ambaye sasa ana kazi ya kurejesha heshima ya Yanga kama ilivyo kwa Phiri ambaye anatakiwa kuhangaika na Simba irudi katika enzi zake.
Uzoefu soka la Bongo:
Phiri ni mzoefu zaidi na soka la Bongo kwa kuwa ameifundisha Simba mara mbili tofauti na mara zote amebeba ubingwa wa Tanzania Bara na ule wa Tusker. Maximo hajawahi kutwaa kombe lolote akiwa na kikosi cha Taifa Stars na hii ni mara yake ya kwanza kufundisha timu barani Afrika kwa ngazi ya klabu.
Phiri anatokea nchi jirani ya Zambia, mazingira yake hayana tofauti na Tanzania. Hivyo hawezi kusumbuka sana, kama ambavyo Maximo atakavyokuwa mgeni kwenye viwanja vya mikoani ambavyo hakuwahi kuvitumia akiwa na Taifa Stars.
Kocha taifa:
Wakati Maximo akiwa na Taifa Stars, Phiri aliifundisha Zambia ‘Chipolopolo’, ameweza kuwa na mafanikio na amefikia ‘levo’ ya juu zaidi kwa kucheza Kombe la Mataifa Afrika (Can) wakati Maximo alicheza michuano midogo ya Chan iliyofanyika Ivory Coast mwaka 2009, Stars ikatolewa na Zambia chini ya kocha Mfaransa.
Takwimu zinaonyesha Phiri ni kocha wa ‘levo’ ya juu zaidi ingawa Maximo anatokea Brazil, barani Amerika Kusini na yeye Afrika.
Wakati Maximo aliipeleka Stars Chan, Phiri akaenda na Chipolopolo Can, bado Mzambia huyo, mwaka 1997 alishiriki Kombe la Dunia la Vijana, michuano iliyofanyika nchini Nigeria akiwa na kikosi cha Zambia.
Rekodi:
Ingawa Maximo hii itakuwa ni mara yake ya kwanza kufundisha soka kwa ngazi ya klabu nchini, tayari Phiri anaweza kuwa na msaada wa rekodi zake zilizopita na zikamuwezesha kufanya kazi kwa uhakika zaidi kwa kuwa amewahi kuchukua makombe zaidi ya mawili.
Rekodi hizo sawa, lakini anajua tabia za wachezaji wa Kibongo na nini cha kufanya katika ngazi ya klabu.
Suala hilo lazima litamsumbua Maximo ambaye hajawahi kubeba kombe lakini kufanya kazi katika ngazi ya klabu na kujua matatizo yake yalivyo.
Pamoja na yote, akizungumza na waandishi wa habari leo, Maximo alimkaribisha Phiri na kusema lazima ajue ugumu wa ligi ya Tanzania na ushindani utakuwa mkubwa.
“Najua Simba wamepata kocha mpya, namkaribisha Tanzania lakini lazima ajue ligi itakuwa na ushindani,” alisema Maximo, jana.
Kuhusiana na Yanga, Phiri alisema siku zote amekuwa akiichukulia mechi dhidi ya Yanga kwa umuhimu zaidi kwa maana ya historia lakini pia kiufundi lazima kushinda.
“Ukishinda unawajenga wachezaji wako kwa maana ya kuinua ari, lakini bado inaongeza hali ya kujiamini. Najua unapata pointi tatu kama mechi nyingine, lakini kushinda mechi hiyo ni bora zaidi na hili liko duniani kote,” alisema Phiri.
Simba inaingia kambini mjini Unguja wakati Yanga chini ya Maximo, nao wataweka kambi kisiwa cha Pemba, wote wakijiwinda na Ligi Kuu Bara msimu wa 2014-15 ambao unatarajiwa kuwa ‘mtamuuuu’.
0 comments:
Post a Comment