Thursday, August 7, 2014

Mpenzi msomaji wangu, ulimwengu wa sasa wa kimapenzi umetawaliwa na sarakasi nyingi sana. Mapenzi ya sasa ni tofauti kabisa na yale ya zamani. Kila mmoja amekuwa na mapenzi ya kisanii, hakuna hata mmoja anayeweza kumfanya mwenza wake akamuamini kwa asilimia zote kwamba ana penzi la dhati.

Yule ambaye wewe unampenda na yeye akakuambia anakupenda sana, bado utakuwa ni mtu wa ajabu kama utasimama mbele za watu na kusema kwa kujiamini kabisa kwamba unapendwa sana na huwezi kusalitiwa.
Nasema utaonekana ni mtu wa ajabu kwa kuwa, huwezi kuwa na ushahidi wa kile unachokisema. Ukiambiwa utoe sababu za kwa nini unaamini hawezi kukusaliti, huwezi kuwa nazo, sanasana utasema ni kwa kuwa anaonesha kukupenda na hujawahi kuona dalili za kwamba anakusaliti.
Hiyo haiwezi kuwa sababu ya wewe kujiaminisha kwamba husalitiwi. Mjanja ni yule ambaye anajua kabisa kuna uwezekano mkubwa mwenza wake anamsaliti lakini akabaki na amani kwa kuwa hajawahi kumfumania wala kuona dalili za kusalitiwa.
Ukisema unaamini mpenzi wako hakusaliti eti kwa kuwa hujawahi kumfumania, hujaona dalili za kwamba anachepuka na anaonesha anakupenda sana, kumbuka wapo ambao walifikia hatua ya kunywa sumu kwa kuwafumania wapenzi wao ambao hawakutarajia wangeweza kuwa na watu wengine nje ya uhusiano wao.
Nasema haya kwa mifano ya wazi kabisa! Yupo rafiki yangu anaitwa Rashida. Huyu nilisoma naye shule ya msingi lakini tukaja kuonana jijini Dar akiwa anafanya kazi karibu na sehemu ninayofanya kazi. Huyu alikuwa na mpenzi wake ambaye walikuwa wanapendana sana.
Alinitambulisha kwa jamaa yake huyo aitwaye Juma, kwa maongezi tu alionekana kuwa mpole sana. Aliongea kwa busara na alionyesha dhahiri kumpenda Rashida. Rashida alifikia hatua ya kuniringisha kwamba, amepita kwa wanaume wengi lakini kwa Juma, amefika.
Akasema anamuamini sana, ametulia sana na anaamini ni mume sahihi wa maisha yake. Alimmwagia sifa kedekede lakini mwisho akanihakikishia kwamba, kwa jinsi anavyoonesha kumpenda, hawezi kusalitiwa na akaniambia kazi ya yeye ni kumdatisha kimahaba ili asifikirie kabisa kutoka nje ya uhusiano wao.
Moyoni nilimsikitikia sana Rashida, ilikuwa hivyo kwa kuwa nilimuona alikuwa na imani sana na Juma. Alimuamini kuliko maelezo na hili lipo kwa wengi walio katika uhusiano.
Kwa kuonesha kuwa nilichokuwa nakiwaza ndicho ambacho kingetokea, juzi alikuja analia. Ilikuwa ni tukio la siku moja tu lakini alikondona sana. Nilipomuuliza akaniambia kuwa, Juma aliyemuamini sana, amemtenda. Amegundua Juma alikuwa na uhusiano na demu mwingine kwa siri.
Mbaya zaidi ni kwamba, msichana aliyekuwa anachepuka na Juma alikuwa akijua kwamba kaingia kwenye uhusiano na mtu ambaye ana mtu wake. Lakini kwa kuwa ameshapenda, akaomba apewe nafasi na yuko tayari uhusiano wao uwe wa siri. Mungu si Athumani, siri ikafichuka!
Tunajifunza nini hapa? Ukweli ni kwamba suala la kusalitiwa lipo tu, tena kwa kila mtu! Nasema hili kwa nia njema kabisa na wala siyo kutaka kuwakatisha tamaa. Huyo uliyenaye tambua kabisa kuna uwezekano anakusaliti kwa siri sana lakini kwa kuwa huna uhakikika, potezea na endelea kumuamini kwa kuwa unampenda.
Nasema hivyo kwa kuwa, kujiaminisha sana kwamba unapendwa na huwezi kusalitiwa kuna madhara makubwa. Wengi waliokuwa na mawazo hayo waliishia kujiua pale walipobaini wanasalitiwa. Ilikuwa ni lazima wajiue kama siyo kuchanganyikiwa kwa kuwa ni jambo ambalo hawakuwahi kulifikiria.
Leo hii ukiwa na mawazo kwamba hakuna asiyesalitiwa, ikija kutokea umegundua mpenzi wako au mume/mke anachepuka, hutaumia sana! Utachukuliwa ni jambo la kawaida na utafanya maamuzi sahihi.
Niseme tu kwamba, mapenzi ya sasa ni pasua kichwa! Kikubwa ni wewe kujua kwamba Mmasai kaingia kwenye disko na sime kiunoni, hivyo ucheze kwa umakini ili sime yake isije ikakudhuru.

0 comments:

Post a Comment

Designed by Adamu Mwanakatwe