Tuesday, July 1, 2014

RIO DE JANEIRO, BRAZIL
KOMBE la Dunia nchini Brazil limefika patamu, lakini mambo ni matamu zaidi Manchester United.
Mageuzi yameshika kasi klabuni hapo baada ya miamba hao ya Old Trafford kuanza kutumia pesa kufanya usajili wa nyota wapya watakaorudisha hadhi ya klabu msimu ujao.
Mabingwa hao mara 20 wa Ligi Kuu England wametumia Pauni 58.8 milioni kuwanasa Luke Shaw na Ander Herrera ikiwa ni mkakati wa kocha mpya, Louis van Gaal, anayepania kuirudisha kileleni timu hiyo baada ya mambo kwenda kombo msimu uliopita.
Hadi kufika jana Ijumaa, Man United ilitarajia kukamilisha uhamisho wa beki wa kushoto, Mwingereza Shaw, ambaye anawagharimu Pauni 30 milioni, hilo likitokea katika kipindi cha saa 24 baada ya kumnasa kiungo wa Athletici Bilbao, Herrera kwa dau la Pauni 28.8 milioni.
Wakati kocha Van Gaal akiwa na majukumu kwenye kikosi cha Uholanzi katika fainali za Kombe la Dunia akijiandaa na mechi za mtoano ambapo kesho Jumapili atamenyana na Mexico, amefurahishwa na Makamu Mwenyekiti wa Man United, Ed Woodward kwa kufanya usajili huo huku ikitarajia kuwanasa mastaa wengine.

0 comments:

Post a Comment

Designed by Adamu Mwanakatwe