
KIBANO! Jeshi la Polisi Changombe, Dar linamshikilia mwanamke aliyetajwa kwa jina moja la Neema na babu Ramadhan kwa RB namba CHA/RB/4645/2014 UNYANYASAJI WA MTOTO wakidaiwa kumsulubu mjukuu wao (jina linahifadhiwa kimaadili).
Tukio la kuwatia nguvuni wahusika hao lilijiri Mei 29, mwaka huu maeneo ya Buza jijini Dar, baada ya ya majirani kusikia kilio cha mtoto huyo akiomba msaada ili kunusuru maisha yake kutokana na kipigo kizito alichodaiwa kupewa na wawili hao.
MAJIRANI WAZINGIRA
Kwa mujibu wa majirani waliozingira nyumbani hao, siyo mara ya kwanza kwa mtoto huyo ambaye ni yatima kupigwa hivyo waliamua kuivamia nyumba hiyo kwa kuwataka wazee hao waache kumpiga mtoto huyo jambo ambalo lilishindikana.
Majirani hao waliokerwa na kitendo hicho walitishia kuchoma moto nyumba hiyo ndipo wazee hao wakaacha kumpiga mtoto huyo na kutoka nje wakijitetea kuwa walikuwa wakimpiga kwa kuwa alifanya kosa.
Walipohojiwa sababu za kumpiga mtoto huyo mara kwa mara, wazee hao walijitetea kuwa mtoto huyo ni mtukutu.
Majirani hao walidai kuwa siku za nyuma wazee hao walishawahi kuandamana kuhusu unyanyasaji wa mtoto huyo ambapo walishawahi kumripoti polisi Chang’ombe.
MAJIRANI WAANDAMANA
Ilielezwa kuwa majirani hao waliripoti kuhusu unyanyasaji huo kwa Mjumbe na Afisa Mtendaji wa eneo hilo, Mary Patrick ambaye alitoa taarifa kwa mwanaharakati wa kutetea haki za watoto kutoka TUHIMIZANE, Cleophace Simioni ambaye alimchukua mtoto huyo na kumpa huduma ya kwanza kabla ya kumpeleka Ustawi wa Jamii kwa ajili ya matunzo.
Waandishi wetu walifika nyumbani hapo na kushuhudia mtoto huyo akiwa na majeraha ya kuchanwa mgongoni, makovu ya moto na uvimbe usoni na kichwani.
Akizungumzia sakata hilo, mwanaharakati huyo alisema atapambana hadi hatua ya mwisho kutetea haki ya mtoto huyo.

Mwishowe wazee hao walifikishwa katika kituo cha polisi Chang’ombe ambapo walifunguliwa shitaka hilo wakisubiri kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
0 comments:
Post a Comment