

Kiukweli limekuwa somo lenye changamoto nyingi sana kutoka kwa watu mbalimbali.
Baadhi wanajiuliza, hivi inawezekanaje kukawa na uongo wenye faida?
Wengi wamehoji, tangu lini uongo ukahitajika kwenye mapenzi? Jibu ni rahisi sana. Ni mara ngapi wewe unayesoma mada hii umedanganya? Bila shaka ni mara nyingi.
Je, umedanganya uongo wa aina gani?
Maana ninachojaribu kujenga hoja hapa ni kwamba tuwe wadanganyifu kwa wapenzi wetu, ila kudanganya inapohitaji kwa lengo la kudumisha mapenzi.
Si vyema kuongopa. Nasisitiza tena, si vizuri kudanganya lakini kama una lengo zuri, hutaki mwenzako akuelewe vibaya, si vibaya kusema uongo ili kulinda penzi lako.
Izingatiwe kuwa, uongo ninaozungumzia hapa si ule mkubwa au unaoweza kusababisha madhara.
Ni mambo madogo ya kawaida yanayotokea katika maisha yetu.
Hebu sasa twende tukaone vipengele vya mwisho vinavyokamilisha mada yetu...
‘MEETING’
Inawezekana upo kwenye ndoa na kwa bahati mbaya jioni wakati wa kurudi nyumbani ulipitia kwenye mambo yako (si usaliti lakini) na pengine hutaki mkeo afahamu kwa sababu zako binafsi.
Ili kukwepa ‘usumbufu’ wake, ukaamua kuzima simu na kuendelea na ratiba zako hadi ulipokuwa sawa na kuanza safari ya kurudi nyumbani.
Mkeo kwa wasiwasi anakuuliza maswali huku akitaka kujua ni kwa nini ulizima simu na mahali ulipokuwa.
Kwa kuwa hukuwa sehemu mbaya na hutaki ajue, uongo wa kumwambia kwamba ulikuwa kwenye kikao unakubalika katika eneo hili.
“Samahani mpenzi wangu, niliingia kwenye meeting (kikao), kilikuwa cha ghafla. Bosi alituita bodi nzima, nisingeweza kuingia na simu ikiwa wazi, lakini unisamehe mama, nilisahau kukujulisha kutokana na presha ya kikao chenyewe, maana kwa sehemu kubwa kilihusu idara yangu.”
Uongo huu utainusuru ndoa yako huku ukiendelea kuwa mwaminifu kwa mwenzako.

Wakati mwingine ili kumfanya mpenzi wako ajisikie kamili unatakiwa kumsifia sana. Kikubwa ni kwamba kutoka ndani ya moyo wako unampenda kwa mapenzi yako yote, msifie kadiri uwezavyo ikiwezekana sifa ambazo hana.
Utakuwa unamdanganya kwamba yeye ni mzuri zaidi ya Miss Tanzania, lakini ukijua kwamba umeridhika naye. Hakuna sababu ya kumuacha akiwa na mawazo, akijifananisha na watu wengine maarufu, akijihisi kwamba pengine hakufai.
Mpe moyo, mwambie boyfriend wako, anakuvutia kuliko mwigizaji fulani mkubwa au msanii wa muziki.
Unajua akianza kujiamini yeye ni bora zaidi ya mastaa wanaozimikiwa na wadada wengi, atakuwa huru zaidi kwako.
Jamaa anaweza kuwa wa kawaida tu, lakini ni wako na upo tayari kuwa naye kwa hali yoyote, kwa nini usimsifie ili muendelee kudumu?
Naamini imetosha sasa, hadi wiki ijayo kwa mada nyingine, USIKOSE!
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Saikolojia ya Uhusiano anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha Maisha ya Ndoa.
0 comments:
Post a Comment