Tangu kutoka bungeni kwa Kundi la Wajumbe wa Umoja wa Katiba ya
Wananachi (Ukawa) kwenye Bunge la Katiba kwa madai ya kuchoshwa kwao na
matusi, kejeli na ubaguzi, kumeibuka mijadala mikali, huku mawaziri na
wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa chama tawala CCM, wakivunja ukimya
na kuamua kupambana na umoja huo kwa hoja kwenye hadhara.
Ni wazi sasa hatua hii inaonyesha bado kuna
mivutano kutokana na kila upande kubeba na kutetea hoja zake na
kutupiana lawama za kuukwamisha Mchakato wa Katiba Mpya.
Wakati Ukawa wakidai wabunge wa CCM ndiyo chanzo
cha kuvuruga na kukwamisha mchakato huo, CCM wanaubebesha msalaba wa
lawama Ukawa na kusema ni wakimbizi wa hoja walioshindwa kujenga
ushawishi na kuamua kuweka mpira kwapani baada ya hoja zao kukosa
mashiko.
Madai ya Ukawa wanaeleza kuwa CCM imeacha kujadili
Rasimu ya Jaji Joseph Warioba iliyowasilishwa bungeni na kuonekana
wakiwa na rasimu yao kibindoni, wakitaka matakwa yao ya kisera na
kiitikadi yapitishwe na Bunge la Katiba kinyume na taratibu.
Ukawa wanakazia msimamo wao na kusema kwamba
Muundo wa Muungano wa serikali mbili si pendekezo la Tume ya Jaji
Warioba iliyowasilishwa katika Bunge hilo maalumu la Katiba.
Hata hivyo, madai mengine ya CCM yanaeleza kuwa
kundi la Ukawa halina nia njema, limeshindwa kujenga ushawishi na
kuonyesha uhalisia wa faida za muundo wa serikali tatu ikiwa ni pamoja
na rasimu ya Warioba takwimu zake kujikanganya na kukosa uchambuzi
yakinifu.
Wadadisi wa masuala ya kisiasa visiwani hapa
wanaeleza kuwa kukwama kwa Mchakato wa Katiba, kunaweza kuendelea
kuiweka Zanzibar katika mzingira magumu ya kiuchumi na kujikuta madai au
kilio chao cha muda mrefu kikakosa mnyamazishaji wa kuwafuta machozi.
Pia wako wanaosema kuwa ni lazima Zanzibar ipate
hadhi yake kamili ili kuwa na polisi wake, uraia, uhamiaji, hati za
kusafiria, elimu ya juu, sarafu na benki kuu yake ili kujitegemea na
kujiendeleza yenyewe.
Hali hiyo pia inapingwa na baadhi ya watu
wanaosema hakuna mahali popote duniani ambapo nchi mbili zimeungana
zikaendelea kuwa na mamlaka kamili na kuyataja madai hayo yana dhamira
ya kuvunja Muungano na kuusambaratisha.
Mifano yao katika kuungana na kubaki na mamlaka moja kamili wanayafananisha mataifa ya Uingereza, Marekani, Ujerumani na India.
Kundi la wabunge wa Ukawa tayari limefanya
mikutano miwili mikubwa ya hadhara katika Kisiwa cha Unguja na Pemba
huku CCM ikifanya mikutano mitatu katika visiwa hivyo kwa nyakati
tofauti wakihimiza msimamo wao kuwa ni sahihi.
CCM imeamua kuwapandisha majukwani mawaziri watano
ili kuwajibu Ukawa wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif
Ali Idd, huku CUF kwa kutumia mwamvuli wa Ukawa, wamewapandisha viongozi
wakuu wa vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema, CUF, NLD , DP na NRA ili
kuweka msimamo wakiongozwa na Makamu wa Kwanza wa Zanzibar Rais Maalim
Seif Sharif Hamad.
0 comments:
Post a Comment