
Ndugu wa damu wakutana kwenye fainali mbili za Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza
JUNI 21 kwenye fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu nchini
Brazil kutashuhudiwa mechi itakayohusisha ndugu wawili wa damu wakiingia
uwanjani kupambana. Hii ni wakati Ujerumani itakapomenyana na Ghana
kwenye mechi za hatua ya makundi ya michuano hiyo.
Ndugu hao wa damu ni Jerome Boateng atakayekuwa
upande wa Ujerumani anashindana na kaka yake Kevin-Prince Boateng
atakayekuwa na kikosi cha Ghana kwenye mechi ya Kundi G.
Wakutana mara ya pili
Kwenye Kombe la Dunia, Jerome na Kevin-Prince
wataendelea kuwa ndugu wa kwanza wa damu kucheza wakiwa timu pinzani.
Wakati mwaka huu kwenye fainali hizo za Brazil wakiwa wamepangwa Kundi G
sambamba na timu nyingine za Marekani na Ureno, mara ya kwanza ndugu
hao kukwaana ilikuwa kwenye fainali za Kombe la Dunia 2010 zilizofanyika
Afrika Kusini.
Mwaka huo, Ghana na Ujerumani zilipangwa pamoja
Kundi D na timu za Serbia na Australia na kwenye mechi yao, Jerome
alitoka kifua mbele kwa ushindi wa bao 1-0, shukrani kwa bao safi la
kiungo Mesut Ozil dakika ya 60, ambaye pia alitajwa kuwa Mchezaji Bora
wa Mechi.
Wote wanacheza Bundesliga
Kuhusu ndugu hao kuwa wapinzani kwenye mechi si
kitu cha ajabu sana baada ya wote kucheza kwenye ligi ya Bundesliga
ambapo timu zao zimekuwa zikichuana mara kwa mara.
Kevin-Prince anacheza kwenye klabu ya FC Schalke
04, wakati mdogo wake ni beki wa kutegemewa wa Bayern Munich, ambao
msimu uliopita walinyakua mataji mawili, ubingwa wa Bundesliga na Kombe
la Ujerumani.
Familia moja kwenye Kombe la Dunia
Fainali za Kombe la Dunia kushuhudia ndugu wawili
wakicheza si kitu cha ajabu. Kwenye fainali za mwaka huu nchini Brazil,
Ivory Coast itakuwa na ndugu kwenye kikosi chake, Kolo Toure na mdogo
wake Yaya Toure.
Kitu kama hicho kiliwahi pia kutokea miaka ya
nyuma wakati Argentina ilipokuwa na ndugu Mario na Juan Evaristo, sawa
na Mexico ilikuwa na ndugu Manuel na Felipe Rosas na Rafael na Francisco
Gutierrez kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka 1930.
Baada ya miaka mingi ikaja zamu ya Fritz na Ottmar
Walter, ambao waliisaidia Ujerumani kuibuka mabingwa nchini Uswisi
1954, kisha wakaja Bobby na Jack Charlton wa England kwenye Kombe la
Dunia 1966 na Robert na Niko Kovac wa Croatia kwenye Kombe la Dunia 2002
nchini Japan na Korea Kusini. Lakini, hawa wote walikuwa wakicheza timu
moja.
0 comments:
Post a Comment