
Dar es Salaam. Wakati Mbeya City wakisaini
mkataba wa udhamini wa miaka miwili wenye thamani ya Sh360 milioni na
kampuni ya Bin Slum Tyre Co. Ltd, wanachama wa Simba wametishia
kumshtaki Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi kwa
Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), kwa madai ya kutaka kumpendelea
mgombea urais wa klabu hiyo, Michael Wambura.
Mapema jana, Mbeya City ilisaini mkataba mnono wa
Sh360 milioni wa kuifanya klabu hiyo kuingiza zaidi ya Sh500 milioni kwa
msimu kutokana na udhamini pekee. Wanapata Sh100 milioni kutoka Azam
Media kutokana na haki za televisheni, huku karibu Sh70 milioni zikitoka
kwa wadhamini wakuu wa Ligi Kuu, Vodacom Tanzania.
Akizungumza wakati wa utiaji saini wa mkataba huo,
mkurugenzi wa Bin Slum Tyre, Mohamed Bin Slum alisema wameidhamini timu
ya Mbeya City baada ya kuona ina uongozi makini na ni timu yenye
mafanikio makubwa.
“Uongozi umejipanga vizuri katika kuendesha timu
yao kupata mwitikio mkubwa kutoka kwa wananchi wa Jiji la Mbeya na mikoa
ya jirani,” alisema Bin Slum.
Naye katibu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe alisema
imekuwa ni faraja kwa timu kwani itaweza kujiendesha na kufanya vizuri
msimu ujao wa Ligi Kuu.
Kimbe alisema Mbeya City ina wajibu wa kuuthamini
mchango huo uliotolewa na mdhamini kwa kuhakikisha inafanya vizuri zaidi
msimu ujao. Kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Dk
Samweli Lazaro alisema malengo ya timu yao ya kubadili mtazamo wa Simba
na Yanga katika soka la Tanzania yametimia baada ya timu hiyo kupata
mdhamini.
Wakati hayo yakitokea Mbeya, hali imekuwa tofauti
kwa vigogo wa soka nchini, Simba baada ya wanachama watano wakiongozwa
na Masoud Hassan (kadi namba 0500), Saleh Shahame (5596), Frank Pastori
(02188), Rajabu Mtibu (01146) na Ally Mkumba (02519) kutishia kwenda
Fifa kumshtaki Rais wa TFF, Malinzi, wakidai ameshatoa maelekezo kwa
Kamati ya Rufaa za Uchaguzi ya shirikisho hilo inayotarajia kukutana
Jumatatu ijayo na kusikiliza shauri la Wambura kupinga kuenguliwa kwenye
uchaguzi wa Simba.
Akijibu madai hayo, Malinzi alisema msimamo wake wa kuitetea na kuilinda katiba na kanuni za TFF na wanachama wake uko palepale.
Malinzi alisema: “Sitegemei kumbeba mtu, ile
kamati ni huru, itafanya kazi yake kwa uhuru kwa mujibu wa kanuni na
katiba na si nje ya hapo.
“Wanaosema nina mpango wa kumbeba Wambura acha
waseme. Ni demokrasia na hata kama wameenda Fifa pia ni sawa. Demokrasia
inawaruhusu, siwezi kuwazuia.”
Wambura, ambaye amekumbana na panga kila
anapojaribu kugombea uongozi wa soka kuanzia ngazi ya klabu hadi taifa,
alienguliwa Simba kwa kuvunja katiba.
0 comments:
Post a Comment