WAGOMBEA wawili katika kiti cha umakamu rais wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ na Sued Nkwabi, inadaiwa ndiyo chanzo cha kutofautiana kwa wanachama wa Tawi la Shibam lililopo Magomeni Mapipa jijini Dar, katika kuamua nani asapotiwe iwapo kampeni zitaanza.
Mmoja wa wanachama hao alilipenyezea Championi Jumamosi kuwa, kumekuwa na mabishano baina yao kutokana na wote kupata sapoti kwa asilimia kubwa.
Aliongeza kuwa mbali na hilo, tayari wanaye rais wao ambaye ni Evans Aveva kwa sababu walizosema kuwa Aveva amekuwa na rekodi nzuri katika uongozi wake Msimbazi ukilinganisha na wagombea wote.
Hata hivyo, kigugumizi kimekuja kumpata msaidizi wake huku wakipigana vikumbo katika ‘promo’ kati ya Nkwabi na Kaburu.
“Unajua suala la uchaguzi ni demokrasia huwezi kumlazimisha mtu. Lakini msimamo wa tawi zima ni Aveva.
“Ila kitendawili kimekuja kwa makamu rais; wapo wanaompigia chapuo Nkwabi, wengine wanasema Kaburu. Mpaka sasa kila mmoja ana msimamo wake kwa hilo lakini si kwa upande wa rais,” alisema mtoa habari wetu
Simba inatarajiwa kufanya Uchaguzi Mkuu Juni 29, mwaka huu, ambapo kiti cha urais kinawaniwa na Aveva na Andrew Tupa, huku Michael Wambura aliyeenguliwa akisubiri hatma yake wiki ijayo baada ya Kamati ya Rufaa TFF kupitia rufani yake.
0 comments:
Post a Comment