Thursday, June 5, 2014



 Marehemu Adam Phillip Kuambiana.
KWENU,Mastaa wa filamu za Kibongo. Najua mna simanzi nzito, bado hali zenu kisaikolojia hazipo sawa kutokana na misiba iliyowakuta hivi karibuni ya kuondokewa na Adam Kuambiana na Recho Haule. Siyo rahisi kupokea, lakini jikazeni, ni kazi ya Mungu.


Marehemu Rachel Haule 'Recho'.
Kuna jambo nataka kuzungumza nanyi ambalo kwa upande mwingine ni funzo kwa wasanii wa tasnia nyingine kama Bongo Fleva, Bongo Dansi na wengineo.
Kwa kawaida, marafiki wa kweli hujulikana kwenye shida, lakini pia hata kwenye raha utaweza kumjua rafiki wa kweli. Kwa maneno mengine naweza kusema, rafiki wa kweli utamjua kwenye shida na raha.
Katika misiba hiyo mmeonyesha kitu kikubwa sana na namna mnavyopendana na kushirikiana kwenye shida na raha.
Hamna unafiki. Sijaona ubaguzi, wote kwa pamoja kama wasanii mmeungana na kuachana na tofauti zote za chinichini mkawasitiri wapendwa wenu.
Nakiri kwamba katika msiba wa Kuambiana, kwa bahati mbaya sikuweza kuhudhuria lakini picha pekee zilionyesha namna ambavyo mlishirikiana na kumzika mwenzenu kwa heshima.
Katika msiba wa Recho, nilipata nafasi ya kushirikiana nanyi. Nakumbuka mimi na wenzangu tukiwa tumeongozana na Mkurugenzi wa Global Publishers, Marsha Bukumbi tulikuja msibani kwa siku tatu mfululizo na kukaa nanyi hadi saa 9 usiku.
Ilikuwa Jumanne, Jumatano na Alhamisi ambapo Recho alizikwa. Kwa kweli lazima niwe mkweli, mlionyesha umoja wenu wa kweli. Mlionyesha namna mnavyoishi kama ndugu. Kila mmoja aliacha shughuli zake na kujiunga msibani.
Naomba niwapongeze wasanii wote mliofika - mastaa na wanaochipukia. Lakini ukiachana na hilo, mlionyesha kitu kikubwa sana kwenye harusi ya mwenzenu Vanitha Omary aliyefunga ndoa na Paul Mtenda ambaye ni Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba akiwawakilisha wasanii nchini.
Niliona wote kwa pamoja mkishirikiana. Hapakuwa na utengano wa TAFF wala Bongo Muvi. Huo ndiyo umoja wa kweli. Ndiyo maana nimesisitiza, urafiki wa kweli huonekana kwenye shida na raha.
Mbali na misiba inayowahusu, hata inapotokea misiba ya wasanii wengine nje ya filamu mmekuwa mstari wa mbele.
Hili liwe funzo kwa wasanii wengine. Urafiki siyo kwenye raha tu, hata kwenye shida.
Narudia tena, poleni kwa misiba na hongereni sana kwa namna mnavyochukuliana matatizo na kushirikiana bila kutengana. Huo ndiyo umoja na upendo wa kweli.

0 comments:

Post a Comment

Designed by Adamu Mwanakatwe