Dodoma.
Bunge la Bajeti linaanza leo mjini Dodoma huku wabunge wakitarajiwa
kuanza kulipwa viwango vipya vya posho, ambazo ni Sh300,000 kwa siku
sawa na kiwango wanacholipwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.
Kabla ya kufikia uamuzi wa kupandisha viwango hivyo kwa Sh100,000 zaidi,
wabunge walikuwa wakilipwa Sh200,000 kwa siku (yaani Sh70,000 kama
posho ya kikao (sitting allowance), Sh80,000 posho ya kujikimu (perdiem)
na Sh50,000 ya gharama za usafiri).
Nyongeza hiyo kwa kila mbunge kwa siku, sawa na asilimia 50,
italigharimu Bunge la Jamhuri ya Muungano kiasi cha Sh18.5 bilioni kwa
siku 52 zilizotengwa kwa ajili ya Bunge la bajeti linalotarajiwa
kuhitimishwa Juni 27.
Januari mwaka 2012, Rais Jakaya Kikwete alikataa maombi ya Bunge ya
kutaka nyongeza ya posho ipande hadi Sh330,000 na badala yake wabunge
hao wakapata nyongeza ya Sh50,000 tu kwa ajili ya usafiri.
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililla alipoulizwa kuhusu nyongeza hiyo,
hakuthibitisha wala kukanusha, lakini akafafanua kwamba hilo ni suala la
uongozi wa Bunge na si la kiutendaji.
“Suala la malipo kuongezeka au kutoongezeka kimsingi siyo kazi ya Ofisi
ya Katibu wa Bunge, vipo vyombo vya juu vya uongozi wa Bunge; Kamati ya
Uongozi na Tume ya Huduma za Bunge, na vyombo vyote vinaongozwa na
Spika. Kwa hiyo, kama kuna nyongeza, sisi tunapewa taarifa tu kwa ajili
ya kutekeleza,” alisema Dk Kashililla na kuongeza:
“Hadi sasa sina taarifa rasmi kuhusu suala hilo, ikiwa litafika mezani
kwangu kama maelekezo, tutatekeleza kwa mujibu wa maelekezo husika.”
Habari ambazo zimelifikia gazeti hili kutoka vyanzo mbalimbali ndani ya
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinasema, uongozi wa muhimili
huo umeamua kuanza kulipa kiasi hicho cha fedha kutokana na shinikizo
kubwa kutoka kwa wabunge.
Taarifa za kuwapo kwa msukumo wa ajenda ya kupandisha posho za wabunge
zilianza kusikika wakati Bunge la Katiba likielekea ukingoni, wakati
wabunge walikuwa wakihoji sababu za wajumbe kulipwa kiasi kikubwa cha
fedha kwa kazi ileile na katika mazingira yaleyale, wakati wabunge wa
Bunge la Jamhuri ya Muungano wakilipwa kiasi kidogo.
“Msingi wa hoja yetu hapa ni kwamba maisha na mazingira ya Dodoma ni
yale sasa, leo kwanini wajumbe wa Bunge la Katiba walipwe Sh300,000 sisi
tulipwe kidogo kuliko hicho?” alihoji mmoja wa wabunge.
“Na usisahau mwanzoni tu pale (mbunge wa Sumve, Richard) Ndassa alitoa
hoja akisema posho hiyo ya Sh300,000 haitoshi kwa kuwa gharama za maisha
Dodoma zimepanda... Gharama haziwezi kupanda Bunge la Katiba pekee.”
Mbunge huyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake, alisema kama kigezo ni
gharama za maisha, mazingira hayo ndiyo wanayokutana nayo wabunge wa
Bunge la Jamhuri ya Muungano.
Spika wa Bunge, Anne Makinda licha ya kutafutwa mara kadhaa hakupatikana
kuzungumzia suala hilo, lakini Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai alikiri
kuwapo kwa msukumo wa wanaotaka nyongeza ya posho, lakini akasema suala
hilo halijafanyiwa uamuzi.
“Hata mimi nimesikia kama ulivyosikia wewe. Ni suala ambalo wabunge
wamekuwa wakilizungumza, lakini uamuzi ni mchakato si suala la mtu
mmoja. Ninavyofahamu mimi uamuzi ulikuwa haujafanyika,” alisema Ndugai.
Utaratibu uliotumika
Awali kulikuwa na taarifa kwamba maombi ya nyongeza ya posho yamepelekwa
kwa Rais Kikwete kwa ajili ya kupata idhini yake, lakini Katibu Mkuu
Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema hakukuwa na maombi ya aina hiyo.
“Kusema kweli maombi hayo sijayaona. Kama yakija tutayashughulikia kwa
mujibu wa sheria na taratibu zilizopo maana ukweli ni kwamba nyongeza
zinategemea uwezo wa Serikali kulipa kwa maana ya bajeti kama ipo,”
alisema Sefue.
Hata hivyo, gazeti hili limethibitishiwa kuwa uongozi wa Bunge
umelazimika kubana sehemu ya matumizi yake katika maeneo mengine hivyo
kuwezesha kupatikana kwa kiasi cha fedha kinachotakiwa kwa ajili ya
nyongeza wakati wa Bunge la Bajeti.
“Bunge lina bajeti yake kwa hiyo walichofanya ni kupunguza matumizi
katika sehemu nyingine kama vile safari na hilo limefanyika, hivyo uwezo
wa kulipa kiasi hicho kinachotakiwa upo,” alisema mpashaji wetu kutoka
ndani ya Ofisi za Bunge na kuongeza:
“Hilo linafanyika kwa kipindi hiki cha Bunge la Bajeti, baada ya hapo
nyongeza hiyo itazingatiwa katika mapendekezo ya bajeti ya 2014/15”.
Mmoja wa maofisa wa Bunge aliliambia gazeti hili kwamba hakukuwa na njia
ya uongozi wa taasisi hiyo kukataa kulipa fedha hizo kutokana na ukweli
kwamba wangepata wakati mgumu kutoa maelezo kwa wabunge.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William
Lukuvi licha ya kukiri kuwapo kwa madai ya wabunge kutaka nyongeza ya
posho, naye hakuwa tayari kulizungumzia kwa undani kwa maelezo kwamba
yeye hakuwapo nchini kwa muda mrefu.
“Mimi kwa kweli nisamehe tu ndugu yangu. Sikuwapo nchini kwa muda maana
nilikwenda nje kwa ajili ya masuala ya afya, hivyo sijapata muda wa
kufahamu kilichozungumzwa na kukubaliwa kuhusu suala hilo,” alisema
Lukuvi.
0 comments:
Post a Comment