Upinzani watoa masharti magumu kushiriki Uchaguzi Mkuu 2015
Katika hotuba hiyo iliyobezwa na wachangiaji wa CCM kuwa imezungumzia Katiba badala ya Bajeti, Mbowe alisema wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), hawatarejea katika Bunge la Katiba mpaka watakapohakikisha kuwa maana halisi ya uwepo wa Bunge hilo unafuatwa.
Dodoma. Serikali imetakiwa kuandaa taratibu za
mpito za kushughulikia Uchaguzi Mkuu ujao ili kunusuru nchi kuingia
katika mtanziko unaoweza kuwa chanzo cha machafuko ya kisiasa, endapo
utafanyika bila kupatikana kwa Katiba Mpya la sivyo Kambi Rasmi ya
haitashiriki.
Hayo yalielezwa jana na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alipokuwa akitoa hotuba ya kambi hiyo
bungeni kuhusu Makadirio ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
“Hatuwezi kuingia uchaguzi wa vitongoji, vijiji na
mitaa kwa utaratibu uliopo leo, hatuwezi kwenda kwenye Uchaguzi Mkuu
mwakani na Tume ya Uchaguzi kama ilivyo leo, hatuwezi tena kwenda kwenye
Uchaguzi Mkuu mwakani wakati matokeo ya uchaguzi wa Rais hayawezi
kuhojiwa mahakamani.”
Aliongeza: “Hatuwezi kuingia kabla na hoja ya
mgombea huru haijapatiwa majibu, tukiwa na daftari la wapigakura
lililopo leo na hatuwezi kulikubali daftari jipya litakalotengenezwa
kama wadau wote hatutashirikishwa kikamilifu.”
Kauli hiyo ya Mbowe imekuja siku moja tu baada ya
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuwasilisha bungeni, Bajeti ya ofisi yake
ambayo imetenga Sh5 bilioni kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa
uliopangwa kufanyika baadaye mwaka huu.
Mbowe alisema kama ilivyo kawaida, Serikali na CCM
inaweza kupuuza tahadhari hizo na kulazimisha kwenda katika chaguzi
hizo katika mazingira ambayo hayana mwafaka kama inavyoonekana sasa
katika Mchakato wa Katiba Mpya.
Ukawa haitarejea bungeni
Katika hotuba hiyo iliyobezwa na wachangiaji wa
CCM kuwa imezungumzia Katiba badala ya Bajeti, Mbowe alisema wajumbe wa
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), hawatarejea katika Bunge la Katiba
mpaka watakapohakikisha kuwa maana halisi ya uwepo wa Bunge hilo
unafuatwa.
Alisema kama lengo ni kutumia mwavuli wa Bunge
Maalumu la Katiba ili kuendeleza mfumo wa kikatiba na muundo wa muungano
uliopo sasa, wajumbe wa Ukawa hawatakuwa sehemu ya usaliti huo kwa
Watanzania.
“Kama kitakachojadiliwa katika Bunge la Katiba
kitalenga kuboresha matakwa ya wananchi kama yalivyodhihirishwa katika
Rasimu ya Katiba na taarifa za tume, wanachama wa Ukawa watakuwa tayari
kurudi kwenye Bunge Maalumu la Katiba ili kuendelea na mjadala wa
rasimu,” alisema Mbowe.
Ofisi ya Rais
Mbowe alisema kati ya wajumbe 201 wa Bunge la
Katiba walioteuliwa na Rais Jakaya Kikwete, zaidi ya wajumbe 160 ni
wanachama wa CCM.
0 comments:
Post a Comment