
Mbeya City
TIMU sumbufu ya Mbeya City leo itaingia vitani kupambana na AFC
Leopards kutoka nchini Kenya kutupa karata yake ya pili kuwania kufuzu
robo fainali ya michuano ya Cecafa Nile Basin inayoendelea nchini Sudan.
Katika mchezo wa kwanza, Mbeya City iliichakaza
Academie Tchite ya Burundi kwa mabao 3-2. Mabao ya Mbeya City yakiwekwa
kiamiani na Paul Nonga, Mwagane Yeya na Temi Felix aliyesajiliwa kutoka
Kagera Sugar wiki iliyopita.
Endapo Mbeya City inayoshiriki michuano ya
kimataifa nje ya mipaka ya Tanzania kwa mara ya kwanza, itaibuka na
ushindi kwenye mchezo huo wa leo itajipatia tiketi ya kucheza robo
fainali ya michuano hiyo.
Mbeya City itacheza mechi yake ya mwisho ya hatua ya makundi dhidi ya Enticelles ya Rwanda kesho kutwa Jumatano.
Kipa wa Simba, Ivo Mapunda amesema endapo timu
hiyo inahitaji kuibuka na ushindi dhidi ya Chui hao wa Kenya wanatakiwa
kujiamini na kucheza kwa kupambana bila kuogopa jina la wapinzani wao.
Ivo ambaye ana uzoefu na timu za Kenya baada ya
kucheza Ligi Kuu ya nchi hiyo kwa miaka miwili alisema, “Leopards ni
timu ya kawaida, hawazidi sana uwezo Mbeya City bali wana uzoefu zaidi
wa michuano ya kimataifa, naamini kama Mbeya City watatulia na kucheza
kwa kujiamini wanaweza kuibuka na ushindi,” alisema Ivo.
Wakati Temi akianza kwa makeke katika timu yake
mpya, Kocha Msaidizi wa Kagera Sugar, Mlage Kabange amesema mshambuliaji
huyo ngongoti ana uwezo wa kuwapiku mastraika waliopo klabuni hapo na
kupata nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza.
Temi aliichezea Kagera kwa miaka 10, alisajiliwa
na Mbeya City mwishoni mwa wiki iliyopita hivyo kujipa changamoto mpya
ya kuchuana na mastraika wengine Saad Kipanga, Mwagane Yeya na Richard
Michael ili kupata nafasi kucheza.
Kabange alikiri kuwa kuondoka kwa Temi kwenye
kikosi cha timu hiyo ni pigo kutokana na uzoefu aliokuwa nao klabuni
hapo na uwezo aliokuwa akiuonyesha msimu hadi msimu hususani katika
upachikaji wa mabao.
Temi aliifungia Kagera Sugar mabao 10 msimu uliopita licha ya kusumbuliwa na majeraha ya hapa na pale.
“Mbeya City na Kagera zina tofauti kidogo halafu
pale Mbeya kuna wachezaji waliotoka na timu mbali na kucheza kwa muda
mrefu kwa pamoja, hiyo ni changamoto kwa Temi ila itabidi aweke bidii ya
kuzoea mazingira na mfumo.
“Ni imani yangu kuwa uzoefu alionao kwenye ligi
kwa takribani miaka 10 sasa utambeba, nadhani hiyo pia ndio sababu kubwa
iliyosababisha Mbeya City kumsajili, ni mchezaji mzuri na anafahamu
kipi cha kufanya kwa wakati gani,” alisema Kabange.
0 comments:
Post a Comment