Migomo Mbeya inaongeza umaskini
Mbali ya kufunga biashara, watu mbalimbali
wakiwamo wageni kutoka wilaya na mikoa mingine wameathirika na matukio
hayo kutokana na kukosa huduma muhimu zikiwamo za usafiri na hata bidhaa
muhimu kwa maisha.
Sababu za kufunga ni kuwapo kwa tishio la vurugu au kwa madai ya kufanya mikutano ya dharura kunakoandamana na migomo baridi.
Kwa mara ya kwanza Februari walifunga maduka baada
ya kufumuka vijana waliokuwa wakizunguka mitaani wakidai wanapinga
mpango wa Serikali kuwataka wafanyabiashara watumie mashine za kutoa
risiti zenye mfumo wa kielektroniki.
Wafanyabiashara walifunga maduka yao kwa siku
mbili na mara ya pili ilitokea Machi kwa madai hayohayo na polisi
walilazimika kupiga mabomu kuwatawanya vijana walikuwa wakitaka kufunga
barabara.
Kana kwamba haitoshi, mwanzoni mwa Aprili
wafanyabiashara walilazimika kufunga maduka yao baada ya vijana wa
bodaboda kuanzisha kizaazaa kwa madai ya kutaka kupambana na polisi
waliokuwa wakimwokoa mtu aliyedaiwa kushiriki kumuua mwendesha pikipiki
maeneo ya Airport jijini hapa.
Nao madereva wa daladala mwishoni mwa Aprili
walikunjua makucha baada ya kusitisha kutoa huduma kwa madai wako kwenye
mkutano wa kujadili sababu za uongozi wa jiji kuwalazimisha daladala
zipitie kwenye Soko la Soweto na eneo la Block T.
Kwa jumla wakazi wa aina mbalimbali katika Jiji la
Mbeya wanaishi maisha yasiyotabirika. Migomo ama vurugu inawazidishia
ukali wa maisha. Wanaofanya maisha yawe mabaya ni wale wanaoshiriki
kuhamasisha wenzao wafunge biashara.
Kufunga biashara ama kuacha kubeba abiria
kunakwamisha mzunguko wa fedha kwa watu mbalimbali. Kama mwenye daladala
alitarajia kupata Sh30, 000 kwa siku husika, akigoma fedha hizo
hazitampitia.
Kwa mfano tukio la mwishoni mwa Aprili daladala
zinazofanya safari kati ya Igawilo, Uyole hadi mjini zilisitisha huduma
kwa siku mbili watu wengi wakiwamo wake wa madereva walilalamika kukosa
fedha.
Hali kadhalika wanafunzi, wafanyakazi walilazimika
kushikilia fedha zao mfukoni ambazo walizipanga kwa nauli zao. Kana
kwamba haitoshi watu wengi waliotaka kununua bidhaa madukani walishindwa
kufanya hivyo kutokana na kukosekana usafiri.
Pia wenye maduka wakiyafunga watambue wazi kwamba wanakosa fedha ambayo hawakuitarajia na kamwe hawataipata tena fedha ile.
0 comments:
Post a Comment