
MANCHESTER United sasa ikae mkao wa kusubiri
mastaa wa maana msimu ujao. Arjen Robben, Thomas Muller, Mats Hummels,
Luke Shaw na Toni Kroos watavaa uzi wa miamba hiyo ya Old Trafford baada
ya jana Jumatatu kusimikwa rasmi kwa Mdachi Louis van Gaal kuwa kocha
mkuu wa kikosi hicho.
Kabla ya kuchaguliwa kuwa kocha klabuni hapo, Van
Gaal alimwambia bosi wa miamba hiyo makamu mwenyekiti, Ed Woodward
orodha ya vitu anavyotaka vifanywe ikiwamo usajili wa mastaa hao makini,
ambao anadai ni lazima wasajiliwe.
Wiki iliyopita, Woodward alisema pesa za kufanya
usajili huo hazina tatizo, zipo tayari na nia ya kufanya hivyo ipo jambo
kwamba wanatazamia kuingia hasara ya pauni 37 milioni kwa msimu ujao
kutokana na kukosa Ligi ya Mabingwa Ulaya ikiwa ni mara ya kwanza tangu
msimu wa 1995-1996 na pia inakosa soka la Ulaya kwa mara ya kwanza baada
ya miaka 25.
Kwenye uteuzi huo, Van Gaal atasaidiwa na mkongwe
wa klabu hiyo Ryan Giggs, ambaye awali alikuwa kocha wa muda baada ya
kutimuliwa kwa David Moyes aliyedumu na miamba hiyo kwa miezi 10 pekee
tangu alipomrithi Sir Alex Ferguson mwaka jana.
Makocha wengine waliokuwa wakihusishwa na kibarua
hicho cha kuinoa Man United ni Carlo Ancelotti na Jurgen Klopp, lakini
uteuzi wa Van Gaal unaweza kupokelewa kwa furaha na mashabiki wa timu
hiyo hasa kutokana na matakwa yake kwamba klabu ni lazima isajili
wachezaji makini wenye hadhi ya kucheza Man United.
Van Gaal ni mfuasi wa soka la kushambulia na hilo
ndilo linalomfanya atake mastaa ambao wataifanya Man United icheze mpira
wa maana msimu ujao na si kubahatisha. Mdachi huyo amesaini mkataba wa
miaka mitatu na miamba hiyo na ataanza kibarua rasmi Old Trafford baada
ya kukiongoza kikosi cha Uholanzi kwenye fainali za Kombe la Dunia
nchini Brazil zitakazoanza mwezi ujao.
0 comments:
Post a Comment