Saturday, May 17, 2014


Mshambuliaji wa Azam FC, John Bocco.

Na adamu mwanakatwe.
JINA la mshambuliaji wa Azam FC, John Bocco na kiungo mkabaji raia wa Ivory Coast, Kipre Balou, ndugu na Kipre Tchetche, yametajwa kuwepo kwenye orodha ya wachezaji wanaohitajika kutua kwenye kikosi cha Yanga.
Majina ya wachezaji hao yalipitishwa na aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Hans Pluijm, raia wa Uholanzi.
Pluijm aliyetarajiwa kuondoka jana Ijumaa jioni kwenda kuanza majukumu yake mapya kwenye Klabu ya Al Shoala ya Saudi Arabia inayoshiriki ligi kuu ya nchini humo, alikuwa akiwahitaji wachezaji hao kwa ajili ya kuimarisha kikosi hicho na ameacha neno kuwa hao ni watu wanaohitajika zaidi.
Taarifa ambazo zimefika mezani mwa Gazeti la Championi Jumamosi zinaeleza kuwa, Mholanzi huyo alikuwa akihitaji straika namba tisa, ambapo akishirikiana na msaidizi wake, Boniface Mkwasa walimpendekeza Bocco kuwa ndiye chaguo la kwanza.
 Kipre Balou ametajwa kuwa chaguo lingine ambapo hasa lengo ni kuziba nafasi ya Frank Domayo aliyetua Azam FC.
“Msimu uliopita, timu yetu haikuwa na straika namba tisa ambaye muda wote anakuwa maeneo ya goli akisubria mpira kutoka kwa viungo.
“Wote tuliokuwa tunawachezesha ni viungo washambuliaji namba saba, 10 na 11 pekee.
“Hivyo, katika kuelekea usajili wa msimu ujao, tumepanga kumsajili mshambuliaji mwenye uwezo mkubwa wa kufunga mabao ili tulimalize tatizo hili,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza:
“Kwa upande wa kiungo mkabaji, tunamtaka mchezaji anayemudu vema kucheza nafasi hiyo mwenye uzoefu mkubwa, tutakayemtumia katika michuano ya kimataifa na ligi kuu.
“Nafasi hiyo tulipanga kuisajili kabla ya kuondoka Domayo kutokana na kiungo huyo kushindwa kucheza vema katika eneo analotakiwa kulicheza.
“Kama Domayo angeendelea kubaki Yanga, basi asingepata nafasi ya kucheza kutokana na benchi la ufundi kumlalamikia kucheza nje ya eneo lake, mwenyewe muda wote unamuona yupo mbele,” alisema mtoa taarifa huyo.
Alipoulizwa Pluijm kuhusiana na usajili wa wachezaji hao alisema: “Nimewaahidi kuifanyia usajili Yanga nikiwa nchini Saudi Arabia katika kuwaboreshea kikosi chao baada ya kuona upungufu uliopo kwenye timu. Lazima apatikane kiungo na mshambuliaji mwenye kiwango kikubwa.”

0 comments:

Post a Comment

Designed by Adamu Mwanakatwe