AZAM KUFURU KUBWA, Yachukua injini ya Yanga, Jangwani wajibu mapigo
Frank Domayo akisaini mkataba wa miaka miwili wa kuichezea timu ya Azam FC msimu ujao, msimu uliopita alikuwa akiichezea Yanga.
INJINI ndio roho ya gari aina yoyote ile, hakuna gari linaloweza
kutembea wala kuwaka kama likitolewa injini. Azam FC imeng'oa injini ya
kikosi cha Yanga.
Imemsainisha straika, Didier 'Mabao' Kavumbagu na
Frank Domayo na sasa imetunisha misuli kwa nyota mwingine mmoja ambao
kama wote waking'ooka tu, Yanga kitanuka.
Jana Jumatano mapema tu Azam ilianza mazungumzo na
kiungo ambaye ni kama injini ya Yanga, Frank Domayo na kiraka Mbuyu
Twite na ilipofika saa 1:30 usiku, ilifanikiwa kuinasa saini ya Domayo.
Domayo ambaye yupo kwenye kambi ya Taifa Stars iliyopigwa Tukuyu, Mbeya
alizungumza na viongozi hao wa Azam mapema na kumalizana kabla ya
kumfuata kwenye kambi ya timu ya taifa na kumsainisha mkataba wa miaka
miwili.
Domayo amemwaga wino kuichezea Azam FC kwa mkataba
wa miaka miwili baada ya kumaliza mkataba wake wa miaka miwili katika
klabu yake Yanga aliyojiunga nayo miaka miwili iliyopita akitokea JKT
Ruvu ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Twite kwa upande wake alikuwa na mazungumzo na
Azam na Yanga jana Jumatano mchana na jioni na alikiri kwamba Azam
wamemuahidi mambo mazuri. Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti imezipata
ni kuwa Azam imepania kuwang'oa nyota hao, lakini Yanga na wenyewe
wameweka mtego kwa kiungo makini wa Azam, Salum Aboubakary 'Sure Boy'.
Hata hivyo, habari za kutoka ndani ya Azam zinabainisha kwamba Sure Boy
ana mkataba wa miaka miwili hivyo itakuwa ngumu kwa Yanga kulipa kisasi
kwa kumsajili kiungo huyo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Meneja wa Azam,
Jemedari Said, alisema kwa mujibu wa ripoti ya Kocha Mkuu wa timu hiyo
Mcamerooni, Joseph Omog, Azam inataka wachezaji sita kwa ajili ya
kukiimarisha kikosi kiweze kucheza kiushindani Ligi ya Mabingwa Afrika
mwakani.
"Katika ripoti ya kocha tuliyoipokea, inaagiza
kuwa tusajili kiungo wa kati mwenye kiwango kikubwa cha kucheza nafasi
hiyo, mawinga wawili kushoto na kulia na kipa mwenye uzoefu wa kimataifa
na hata beki wa pembeni hasa kulia.
"Yupo Manula (Aishi) mwenye uwezo mkubwa, lakini
yeye hana uzoefu wa kucheza mechi za kimataifa, hivyo tunaendelea na
usajili wetu wa kimya kimya kama tulivyofanya kwa Kavumbagu," alisema
Jemedari ambaye aliwahi kuichezea Simba.
Kavumbagu aliiambia Mwanaspoti kuwa hatashangaa
akisikia Twite amesaini Azam kwa vile Yanga bado hawaeleweki na amekuwa
karibu na Twite anajua kila kinachoendelea.
Twite alipotafutwa kuzungumzia hilo, alisema:
"Kiukweli kabisa, Azam nimepanga kukutana nao leo (jana Jumatano) jioni
kwa ajili ya kusaini mkataba wa kuichezea timu hiyo.
"Yanga wameniita nimepanga kukutana nao kwa ajili
ya mazungumzo ya kusaini mkataba mpya, majibu kamili nitayatoa mara
baada ya kukutana nao wote."
Hata hivyo Twite na alipotafutwa baadaye jioni, akasema kwamba hawajafikia muafaka.
0 comments:
Post a Comment