Tukuyu Stars: Waliinusuru Simba kushuka daraja, sasa choka mbaya
JINA la Tukuyu Sars linapotajwa linawakumbusha mambo mengi wapenda soka nchini.
Ni jina la timu ya soka kutoka wilayani Rungwe
mkoani hapa ambayo iliwashangaza wapenzi wa soka nchini hususan wale wa
Simba na Yanga ilipopanda Ligi Daraja la Kwanza (sasa Ligi Kuu) na
haikukamatika hadi kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara.
Tukuyu Stars ilifanya maajabu hayo mwaka 1986
lakini sasa inatapatapa kwenye ligi Daraja la Tatu mkoa, inahaha ili
ipande daraja na kuungana na timu za Prisons na Mbeya City za mkoani
Mbeya ambazo zinashiriki Ligi Kuu.
Michuano ya Ligi Daraja la Tatu Mkoa ilimalizika
hivi karibuni ikishirikisha timu sita, Tukuyu Satrs ilishika nafasi ya
tatu na kuiacha Timu ya Wenda ikipanda daraja kuingia la pili.
Katika michuano hiyo Tukuyu Stars ilishinda mechi mbili na kutoka sare mara moja na kufungwa mechi moja.
Juhudi za Tukuyu na mashabiki wa timu hiyo kuhakikisha inapanda hadi Ligi Kuu bado hazijafanikiwa kutokana na matatizo lukuki.
Moja ni ukweli kwamba timu hiyo kwa sasa haina
uongozi wa kueleweka. Wachezaji wanajiongoza na kujisimamia wenyewe ili
kulinda heshima ya Jina la Tukuyu Stars.
Kocha mchezaji Josiah Steven ambaye pia ndiye kipa wa timu hiyo anakiri kwamba timu yake inakabiliwa na hali ngumu.
“Kwa mfano michuano ya Ligi Daraja la Tatu
tumeimaliza kwa wachezaji kujitegemea chakula nyumbani kwao na hata
nauli wanatumia za kwao. Muda mwingine tunatembeza bakuli kuomba fedha
za mafuta tunapopata gari. Tunacheza mechi bila ya kuwa na maji ya
kunywa,’’ anasema kocha huyo.
Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Crispin Meela anakiri kwamba Tukuyu Stars ya sasa ni kama watoto yatima kwani hawana viongozi.
Anasema uongozi wa serikali ya wilaya umetoa
maelekezo kwamba, nguvu mpya zitaingia baada ya timu hiyo kupata uongozi
kamili na unaoaminika.
Mmoja wa wachezaji wa timu hiyo, Richard Businge amesema timu yao ingepata msaada wa kifedha ingeweza kupanda daraja mara moja.
0 comments:
Post a Comment