RAMSEY IS BACK: Yupo tayari kuivaa Everton
LONDON, ENGLAND
WALAU mashabiki wa Arsenal na kocha wao, Arsene
Wenger, wanaweza kupumua kama kiungo, Aaron Ramsey, atarudi uwanjani na
kiwango kilekile alichokuwa nacho wakati wa raundi ya kwanza ya Ligi Kuu
England.
Wenger ametangaza kwamba kiungo huyo wa kimataifa
wa Wales, anatarajiwa kurudi uwanjani kesho Jumapili katika pambano
muhimu la kwania kuingia Top Four dhidi ya Everton litakalofanyika
uwanjani Goodson Park jijini Liverpool.
Ramsey hajaichezea Arsenal mechi yoyote tangu
Desemba 26 mwaka jana wakati walipoibamiza West Ham mabao 3-1 na
alitarajiwa kuwa nje kwa wiki sita kutokana na maumivu ya misuli ya
paja, lakini muda huo ukaongezeka baada ya kujitonesha wakati akiwa
katika harakati za kurudi uwanjani.
Nyota ya Ramsey msimu huu imeng’ara kwa kiasi
kikubwa na katika raundi ya kwanza alikuwa amefunga mabao 13 ya Ligi Kuu
England na tangu alipoumia Arsenal imeyumba kwa kiasi kikubwa katika
eneo la ushambuliaji.
Beki wa pembeni wa Arsenal, Nacho Monreal, naye
anaweza kucheza Goodison Park huku kiungo Abou Diaby ambaye yuko nje ya
uwanja karibu mwaka mmoja sasa akikaribia kurudi baada ya maumivu
makubwa ya goti.
“Aaron na Nacho Monreal wamerudi katika mazoezi,
hizo ni habari nzuri. Nina matumaini watapatikana Jumapili. Diaby
amerudi uwanjani kwa hiyo na hizo ni habari njema,” alisema Wenger.
Viungo Jack Wilshere na Mesut Ozil bado wako nje
ya uwanja, lakini beki wa kati Laurent Koscielny anaweza kurudi wiki
ijayo katika pambano la nusu fainali ya Kombe la FA dhidi ya Wigan. Hiyo
ni baada ya kuanza kupata nafuu katika maumivu ya kiazi chake cha mguu.
Wenger amekiri kwamba itakuwa mapema kumrudisha
Ozil katika pambano dhidi ya Wigan, lakini Ozil mwenyewe ameandika
katika ukurasa wake wa Facebook kuwa amepania kurudi uwanjani akiwa
katika kiwango na kwa wakati mwafaka.
0 comments:
Post a Comment