IGP Mangu apangua makamanda polisi
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Ernest Mangu.
Dar es Salaam. Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini,
IGP Ernest Mangu amefanya mabadiliko ya baadhi ya makamanda wa mikoa,
wakuu wa upelelezi wa mikoa, wakuu wa usalama barabarani wa mikoa pamoja
na watendaji wengine wa vikosi na vitengo mbalimbali ndani ya jeshi
hilo.
Mmoja wa waliokumbwa na mabadiliko hayo ni Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi (ACP) Peter Ouma ambaye
amepelekwa Makao Makuu ya Polisi, nafasi yake kuchukuliwa na aliyekuwa
Ofisa Mnadhimu Mkoa wa Dodoma, (ACP) Suzan Kaganda.
Ouma amehamishwa zikiwa zimepita siku 10 tangu
magari 1,000 kukwama kwenye Barabara Kuu ya Mwanza kwenda Dar es Salaam
katika Kijiji cha Ngonho, Kata ya Miguwa, wilayani Nzega mkoani humo,
kutokana na utekaji wa malori.
Katika tukio hilo, madereva waligoma kuondoa
magari kutokana na kuchukizwa na kitendo cha polisi wa eneo hilo
kushindwa kupambana na ujambazi, na ilibidi Ouma afanye kazi ya ziada
kuwabembeleza.
Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Polisi jana,
Advera Senso ilieleza kuwa mabadiliko hayo ni ya kawaida na lengo lake
ni kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma bora ya usalama.
Makamanda wa mikoa
Taarifa ilieleza kuwa aliyekuwa Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Ruvuma (RPC), SACP Deusdedit Nsimeki amehamishiwa mkoani
Manyara, ambako aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, ACP Akili
Mpwapwa amekuwa RPC mkoani Ruvuma.
Mwingine ni aliyekuwa Ofisa Mnadhimu Mkoa wa Lindi, (ACP) Renatha Mzinga ambaye amekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi.
Idara ya Upelelezi
Aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mtwara, ACP
Eliyakimu Masenga amepelekwa kuwa Mkuu wa Upelelezi Kikosi cha Tazara
kushika nafasi ya SP Isack Msengi anayekuwa Kaimu Mkuu wa Upelelezi Mkoa
wa Pwani.
“Aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Tabora, ACP
David Mnyambuga anakuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Ilala kushika
nafasi ya ACP Juma Bwire anayekuwa Ofisa Mnadhimu Mkoa wa Tabora,”
inaeleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa aliyekuwa Ofisa
Mnadhimu Mkoa wa Tabora, (SSP) John Kauga anakuwa Mkuu wa Upelelezi
mkoani humo wakati aliyekuwa Mkuu wa Polisi Wilaya ya Rombo, SSP Ralph
Meela anakuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mtwara.
0 comments:
Post a Comment